Skip to main content
Habari na Matukio

WAZIRI WA KILIMO AKUTANA NA RAIS WA SHIRIKISHO LA VYAMA VYA USHIRIKA DUNIANI

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) Jana tarehe 21 Januari 2019 katika ukumbi wa Wizara ya Kilimo maarufu (Kilimo I) Mtaa wa Tazara Jijini Dar es salaam amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Shirikisho la vyama vya Ushirika Duniani (ICA) Dkt Ariel Guarco.

 

Katika mkutano huo uliotanguliwa na ziara ya kutembelea maeneo mbalimbali ya vyama vya Ushirika Jijini Dar es salaam Rais huyo ameambatana Mkurugenzi Mtendaji wa Shirikisho hilo Ndg Bruno Roelants pamoja na Rais wa Shirikisho la vyama vya Ushirika Afrika Ndg Japhet Magomere na Katibu Mkuu wa Shirikisho la hilo barani Afrika Bi Chiyoge Sifa

 

Pamoja na mambo mengine Mhe Hasunga amemuhakikishia kiongozi hugyo wa Shirikisho hilo kuwa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe Rais Dkt John Pombe Magufuli imedhamiria kuboresha mapungufu ya muda mrefu kwenye vyama vya Ushirika ikiwemo kushughulikia viongozi wabadhilifu.

 

Hasunga alisema kuwa serikali kupitia Wizara ya Kilimo ipo katika mapitio ya sifa za viongozi wa Vyama vya Ushirika nchini ili kupata viongozi watakao ongoza kwa weledi sekta ya Ushirika.


 

Alimueleza Rais huyo kuwa Dhana ya kuchagua viongozi wa ushirika wenye sifa ya kujua kusoma na kuandika imepitwa na wakati hivyo kuna kila sababu ya kuchagua viongozi wenye weledi na utashi katika utendaji.


 

Aliongeza kuwa mfumo wa ushirika  ni nyenzo muhimu ambayo ukitumika vizuri itasaidia kuondoa  umaskini wa wakulima hapa nchini na Dunia kote utaimarisha uanzishwaji wa viwanda kuleta tija katika kilimo hivyo ni lazima kuwa na juhudi za makusudi kuwa na viongozi wenye weledi.


 

Alisema kuwa Wizara yake pia imeanza kupitia upya sheria ya vyama vya Ushirika ili kuwa na Ushirika imara na wenye nguvu na tija kwa wakulima kwani kufanya hivyo kutaongeza Imani ya wananchi waliokata tamaa na Ushirika.

 

Alisema pia miongoni mwa changamoto zinazoikabili sekta ya Ushirika nchini ni kukosekana kwa taarifa sahihi za wanachama (Data Base) kuanzia vyama vya msingi (Union) hadi vyama Vikuu vya Ushirika (AMCOS) jambo ambalo kwa muda mrefu limepelekea kuwa na Ushirika usiokuwa na tija na manufaa kwa wakulima wanaotumia nguvu na rasilimali zao nyingi katika kilimo.

 

Naye, Rais wa Shirikisho la vyama vya Ushirika Duniani (ICA) Dkt Ariel Guarco amesema kuwa msingi wa ziara yake hiyo katika Afrika Mashariki pamoja na nchi zingine ni sehemu ya utekelezaji wa wajibu wake ambapo alianzia Kenya, Rwanda na sasa Tanzania.

 

Alisema kuwa Tanzania ni miongoni kwa nchi zilizopo chini ya Jangwa la Sahara ambayo imepokea vyema dhana ya Ushirika ambapo serikali inaunga mkono kwa kiasi kikubwa hivyo ana Imani miaka michache ijayo kupitia mfumo huo wakulima watakuwa na mafanikio yasiyopimika.

 

Alisema kuwa amezuru nchini Tanzania kwa ajili ya kuonana na kufanya mazungumzo na wana Ushirika ikiwa ni sehemu ya kubaini na kuzitafutia ufumbuzi wa haraka changamoto mbalimbali kwenye sekta ya Ushirika. Vilevile ameeleza kuwa ziara hiyo ni sehemu ya kuendeleza na kuimarisha uhusiano uliyopo baina ya Tanzania na Shirikisho hilo.

 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Shirikisho la vyama vya Ushirika Tanzania (TFC) Bi Aberhad Mbepera alisema kuwa ziara ya Rais huyo ni sehemu ya ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na ICA.

 

Alitoa wito kwa wakulima kujiunga na vyama vya Ushirika kwani katika Ushirika kutaimarisha umoja na mshikamano kwa kufanya kazi kwa bidii na kuwa na kauli moja katika kupanga bei ya bidhaa zao pasina kugalalizwa.

 

Akitoa neno la shukrani Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika nchini Dkt Titus Kamani alisema kuwa maisha ya watanzania yataimarika kupitia Ushirika hivyo Tume hiyo imejipanga kutoa elimu kwa wakulima nchini kuelewa umuhimu wa kujiunga na mfumo wa Ushirika.

 

Alisema Ushirika ni nyenzo pana katika maisha halisi ya wananchi kwani hatua mbalimbali za wananchi zinategemea Ushirika kuanzia maisha ya kawaida, biashara na kilimo.

 

Aliongeza kuwa Tume ya Maendeleo ya Ushirika imedhamiria kuwanufaisha watu masikini kuwa na kipato cha kati kitakachomudu ukali wa maisha na kuwa na utajiri. 

 

MWISHO.