Skip to main content
Habari na Matukio

Mh. Hussein Bashe ahudhuria Mkutano Mkuu wa nchi 25 zinazozalisha Kahawa Afrika, nchini Kenya

Waziri wa Kilimo Hussein Bashe  amefanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Shirika la Wazalishaji Kahawa Afrika(InterAfrican Coffee Organization-IACO) Balozi Solomon Rutega, Jijini Nairobi nchini Kenya, wakati wa Mkutano Mkuu wa nchi 25 zinazozalisha Kahawa Afrika, (G 25 Africa Coffee Summit). 

Tanzania na IACO zitashirikiana katika masuala makuu matatu, ikiwa ni pamoja na, Kuanzisha kituo cha ubora cha Kahawa Jijini Dodoma, Kuanzisha kampeni ya unywaji kahawa katika soko la ndani na kuimarisha uhusiano katika Utafiti na Maendeleo ya zao la Kahawa. 

“Tanzania itakuwa mstari wa mbele kuhakikisha makubaliano haya yanatekelezwa kwa ufanisi pamoja na kuendelea jitihada za kukuza tija katika zao la kahawa na kuboresha pato la mkulima” amesema Waziri Bashe. 

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Balozi Rutega ameonesha utayari wake wa kushirikiana na Tanzania kwa kufika nchini na kukutana na wadau wa kahawa.

Pia amepokea pendekezo la Waziri Bashe lililotaka Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano wa tatu, utakaofanyika mwaka 2024.

“Nashukuru sana Waziri kwa ushirikiano wako wa kukuza sekta ya kilimo Tanzania  na kubadilisha mtazamo wa sekta ya kilimo kwa vijana, sisi tuko tayari kushirikiana nawe katika jitihada zako za kupambania kukua kwa sekta ya kilimo na hasa zao la kahawa” amesema Balozi Rutega

Waziri Bashe katika mkutano huo ameongozana na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Mazao Bw. Nyasebwa Chimagu na Mkurugenzi wa Bodi ya Kahawa Bw Primius Kimaryo