Skip to main content
Habari na Matukio

WAZIRI WA KILIMO PROF. MKENDA AIPONGEZA TARI KWA KUTEKELEZA AGIZO LA WAZIRI MKUU KUHUSU UZALISHAJI W

WAZIRI WA KILIMO PROF. MKENDA AIPONGEZA TARI KWA KUTEKELEZA AGIZO LA WAZIRI MKUU KUHUSU UZALISHAJI WA MICHE YA MICHIKICHI

Waziri wa Kilimo Mhe. Prof. Adolf Mkenda ameipongeza Taasisi ya Utafiti wa Mazao ya Kilimo (TARI) kwa kutekeleza agizo la Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa alilolitoa tarehe 28 Julai, 2018 baada ya kufanya kikao na Wadau kuhusu kuzalisha mbegu bora na miche ya michikichi; Lengo ni kuongeza upatikanaji wa mafuta ya kula nchini kupitia uendelezaji wa zao la chikichi mkoani Kigoma.

Prof. Mkenda amesema; Agizo la Waziri Mkuu linapaswa kutekelezwa kwa nguvu zote kwa kuwa Tanzania ina ardhi ya kutosha pamoja na utaalam wa Watafiti utaokoa fedha nyingi ambazo Serikali imekuwa ikitumia zaidi ya nusu tilioni, kuagiza mafuta ya kula kutoka nje ya nchi kila mwaka.

“Uzalishaji wetu wa ndani wa mafuta ni asilimia 36 tu kiasi kingine kilichobaki kinaagizwa kutoka nje; Huu ni wakati wa kufanya kwa vitendo kuongeza uzalishaji na tija kwenye zao la chikichi kwa kuwa ardhi nzuri tunayo na nia ya kufanya tunayo”.

“Tuna kila sababu ya kuokoa kiasi cha fedha zaidi ya biloni 443 ambazo Serikali ilitumia mwaka uliopita; Mahitaji ya mafuta ya kula nchini ni tani 570,000 kila mwaka ambapo uwezo wa nchi kuzalisha ni tani 205,000 sawa na asilimia 36% na kuongeza kuwa kiasi cha tani 365,000 sawa na asilimia 64 ya mafuta uagizwa toka nje.” Amekaririwa Waziri Prof. Mkenda.

Waziri Prof. Mkenda ameongeza kuwa Serikali imeamua kuanza na mkoa wa Kigoma na kuongeza kuwa zaidi ya mikoa 16 imeonesha fursa ya kupanda zao la chikichi.

“Napenda mfahamu kuwa mkoa wa Kigoma umekuwa njia ya kuanzia kuelekea mapinduzi makubwa ya kuongeza tija na uzalishaji kwenye zao la chikichi.”

“Nitoe wito kwa Wananchi wa mkoa wa Kigoma kulipokea na kulichangamkia zao la chikichi; Mkoa wa Kigoma umeendelea kuimarika kwenye Sekta ya Mawasiliano, njia za mawasiliano zimefunguka, tunataraji baada ya muda mfupi, tutaanza kuona matunda ya zao la chikichi.”

“Nitoe wito kwa Halmashauri sita za mkoa wa Kigoma na Wakulima kuendelea kuzalisha miche ya kutosha kupitia mbegu bora hizo zilizozalishwa na kutolewa na Kituo cha TARI Kihinga kuzipokea, kuzipanda na kuzilinda kwa kuwa miche ya chikichi inapendwa na wanyama kama mbuzi na kondoo.” Amekaririwa Prof. Mkenda.

Katika Taarifa yake kwa Waziri wa Kilimo; Mkurugenzi Mkuu wa TARI Dkt. Geoffrey Mkamilo amesema hadi sasa kiasi cha mbegu 1,863,111 zilisambazwa kwa Taasisi nyingine za Umma na Sekta Binafsi ambapo miche 1,087,143 imezalishwa kutokana na mbegu hizo.

Prof. Mkenda ameongeza kuwa amekuja mkoani Kigoma kwa ajili ya kumpokea Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ameshawasili mkoani Kigoma kwa ajili ya kuanza ziara ya siku mbili.

“Tumekuja mkoani Kigoma kwa ajili ya kujiunga kwenye ziara ya Waziri Mkuu; Mhe. Kassim Majaliwa ambaye atatembelea na kugagua shughuli za maendeleo ya Sekta ya Kilimo hususan zao la chikichi. Tupo tayari kumuonyesha nini kilichofanyika na wakati huo huo, kupokea maelekezo yake mapya.” Amekaririwa Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda.