Skip to main content
Habari na Matukio

WAZIRI WA KILIMO PROF. MKENDA AKABIDHI MAGARI MANNE KWA WARAJIS WASAIDIZI

WAZIRI WA KILIMO PROF. MKENDA AKABIDHI MAGARI MANNE KWA WARAJIS WASAIDIZI

Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Makenda leo tarehe 6 Januari, 2021 amekabidhi wa magari manne aina ya Nissan Hard N 300 Double Cabin 4WD yenye thamani ya Shilingi 275,091,670/- kwa pamoja kwa Warajis Wasaidizi wa mikoa minne. Mikao hiyo ni Simiyu, Kilimanjaro, Njombe na Dar es Salaam.

Waziri wa Kilimo Prof. Mkenda pia amekabidhi kompyuta 25 pamoja na printa moja (1) zenye thamani ya Shilingi 49,050,000/- kwa ujumla; Katika hotuba yake kwa Washiriki wa hafla hiyo. Waziri Mkenda amesema magari na kompyuta alivyowakabidhi leo Warajis Wasaidizi wa mikoa zikatumike kuongeza kasi ya uwajibikaji kwa Watumishi walioko katika maeneo mbalimbali nchini ili kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.

Waziri Mkenda amesema vitendea kazi hivi ni kwa ajili ya kuimarisha shughuli za utendaji kwa lengo la kuboresha kasi ya utendaji kazi kwenye usimamizi wa Vyama vya Ushirika.

“Hakikisheni vitendea kazi hivi vinatunzwa ipasavyo na kutumika vizuri ili kufikia malengo yaliyokusudiwa. Aidha, naagiza Ofisi ya Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika isimamie ipasavyo matumizi na matunzo ya vifaa hivi kwa kufanya ufuatiliaji wa mara kwa mara”. Amekaririwa Waziri Mkenda.

“Kwa kuwa ninyi ni wasimamizi wa Vyama vya Ushirika katika ngazi ya mikoa, nawaagiza kutekeleza ipasavyo Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 – 2025 ambayo imetoa maelekezo mahsusi ya kutekelezwa katika Sekta ya Ushirika.”

“Kila mmoja wenu aisome na kuielewa Ilani ya Chama Tawala, hasa Aya ya 34 inayosema: “Katika kipindi cha miaka mitano (2020 - 2025). Chama Cha Mapinduzi kitahakikisha dhana ya Ushirika wa hiari inajengwa na kusimamiwa na sheria ili kuwalinda na kuwanufaisha Wanaushirika, hivyo kuchangia ipasavyo katika ustawi wao na Taifa kwa ujumla. Ni Imani yangu kuwa wakati wote mtakuwa tayari kutoa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM katika maeneo yenu kwenye ngazi ya mikoa na wilaya zenu. Vifaa ninavyowakabidhi leo ni chachu ya kuwawezesha utelekelezaji wa maelekezo haya ya Chama na Serikali.” Amesisitiza Waziri Mkenda.

Waziri Mkenda amempongeza Mrajis Mkuu na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika kwa kukusanya mapato ya Tume na kununua magari manne yenye thamani ya shilingi 275.

“Ninafahamu kuwa vitendea kazi ninavyowakabidhi leo ikiwemo magari kwa ajili ya usafiri wa Watumishi katika kutekeleza majukumu yao havitatosheleza kwa wote; magari haya manne (4) yanakabidhiwa kwa mikoa minne (4) hivyo kufanya mikoa yenye magari kwenye Ofisi za Tume kuwa sita (6).”

“Hivyo basi, jumla ya mikoa ishirini (20) bado itabakia kuwa haina magari. Naomba niwahakikishie kuwa Serikali kwa kushirikiana na Wadau wa maendeleo itaendelea kuboresha mazingira ya kufanyia kazi kwa Watumishi wa Sekta hii muhimu kwa kuendelea kununua magari zaidi na kuongeza vitendea kazi vingine ili kuimarisha usimamizi Ushirika nchini.” Amemalizi Prof. Mkenda.