Skip to main content
Habari na Matukio

Wekeza katika Kilimo Kuongeza Uzalishaji na Tija – Patrick Otto

Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) nchini Bwana Patrick Otto alisema njia pekee ya kupambana na umaskini ni kwa nchi Wanachama, duniani kote kuwekeza katika kilimo ili kuongeza tija na uzalishaji.


Takribani watu milioni 800 duniani kote, wengi wao wakiwa wanatoka Vijijini, hawana chakula cha kutosha na wanakabiliwa  na utapiamlo mkali huku zaidi ya watu bilioni moja wanaishi katika umaskini mkubwa.
Bwana Otto aliainisha juhudi ambazo FAO kwa kushirikiana na Serikali imekuwa ikifanyakatika kuendeleza kilimo nchini. Aliutaja Mpango wa Kuendeleza Kilimo unaojulikana kama Country Programming Framework – (CPF), chini ya Mpango huo, FAO  imeanza kusaidia katika eneo la kuendeleza kilimo cha biashara, maliasili na mazao yake na kuweka mipango endelevu katika kilimo na kuvutia uwekezaji.

Bwana Patrick alikaririwa akisema “Siku ya Chakula Duniani mwaka huu iwe ni fursa ya kutafakari juu ya malengo huku nchi 193 zimekubaliana na ajenda mpya ya maendeleo  endelevu hususan kukomesha njaa duniani kote ifikapo mwaka 2030”.

Maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani mwaka huu, yalikwenda sambamba na tukio la upandaji miti 70 ya matunda katika Viwanja vya Shule ya Somanda A na B. 
Shughuli hiyo ilifanywa kwa ushirikiano wa uongozi wa Mkoa wa Simiyu, Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika na Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi lengo likiwa kuweka kumbukumbu ya miaka 70 ya FAO.
Huu ni mwaka wa 35 tangu dunia ianze kuadhimisha, Siku ya chakula duniani ambayo hufanyika ifikapo tarehe 16/10 kila mwaka. Maadhimisho ya mwaka huu yanaenda sambamba na maadhimisho ya miaka 70 ya FAO. Kaulimbiu ya maadhimisho ya Siku ya Chakula kwa mwaka huu inasema; Kilimo na Hifadhi ya Jamii katika kuondoa Umaskini Vijijini.