Skip to main content
Habari na Matukio

WFP KUSHIRIKIANA NA SERIKALI KUTAFUTA SOKO LA NAFAKA NJE-BASHE

WFP KUSHIRIKIANA NA SERIKALI KUTAFUTA SOKO LA NAFAKA NJE-BASHE

 

Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limekubali kuwa na ushirikiano na Wizara ya Kilimo katika kutafuta soko lauhakika la mazao ya mahindi na mtama nje ya nchi.

Kauli hii imetolewa jana na Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe mara baada ya kufanya mazungumzo ofisini kwake na Mwakilishiwa Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Chakula Duniani Michael Dunford.

Mhe.Bashe amebainisha kuwa Wizara ya Kilimo inamkakati wa kuhakikisha mahindi na mtama unaozalishwa nchini unapata soko la uhakika ili kuinua uchumi wa wakulima

“Wizara inataka kutumia uzoefu wa Shirika la Chakula Dunia katika kuyafikia masoko ili mazao ya wakulima wetu yaweze kupata bei nzuri katika soko la Afrika” alisema Naibu Waziri

Amewahakikishia WFP kuwa wizara imejipanga kuona uzalishaji wa mahindi na mtama unaongezeka na kuzingatia kiwango cha ubora kinachotakiwa na soko la nje.

Aliongeza kuwa kwasasa serikali kupitia Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko na Wakala waTaifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) wamewezeshwa ili wanunue na kuhifadhi nafaka kwa wingi na kwa kuzingatia viwango vya kimataifa.

“Ni lengo la wizara kuhakikisha wakulima nchini wanaunganishwa na fursa za masoko ya mazao yao ili uchumi wa nchi uendelee kukua kwakasi kupitia sekta ya kilimo” alisema Bashe

Naibu Waziri Bashe alisema mkakati wa wizara katika kipindi cha miaka mitatu ijayo ni kuona Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko inakuwa na uwezo wa kuhifadhi kisasa nafaka tani 520,000 tofauti na ilivyosasa ambapo tani 120,000 zinahifadhiwa,hivyo kuwa na uwezo wa kuuza nje.

Kwa upande wake mwakilishi wa Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Chakula Duniani Michael Dunford amesema wanahitaji kununua zaidi ya tani 50,000 za mahindi toka Tanzania kwa ajili ya kusaidia nchi za Uganda na Sudan Kusini.

Dunford alisema kutokana na uzalishaji mzuri ulipo Tanzania kwenye zao la mahindi unatoa fursa ya soko la uhakika endapo vigezo vya ubora unaotakiwa na Shirika la Chakula Duniani utazingatiwa ikiwani pamoja na kupunguza tatizo la sumukuvu.

Ameishauri wizara ya kilimo kutumia uzoefu na teknolojia ya kisasa uliopo WFP katika kudhibiti upotevu wa mazao baada ya mavuno ili wakulima wapate ufanisi katika uzalishaji.

“Tanzania inapoteza asilimia 30 ya mazao ya wakulima baada ya mavuno kutokana na kukosekana kwa uhifadhi bora na teknolojia ya kisasa” alisemaDunford

Katika kuhakikisha ushirikiano huu unafikiwa,Dunford alisema Shirika la Chakula Duniani linahudumia chakula kwa watu zaidi ya milioni 150 wenye uhitaji katika maeneo yenye migogoro na majanga ,hivyo Tanzania inayofursa ya kupatasoko la nafaka .

MWISHO