Skip to main content
Habari na Matukio

WIZARA YA KILIMO IMEGAWA DAWA NA MBEGU KWA WAKULIMA

Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe  amesema Wizara ya Kilimo imegawa mbegu za Pamba na Dawa bure kwa Wakulima wa Pamba wa Wilaya ya Biharamuri mkoani Kagera.

Waziri Bashe Ameyasema hayo wilayani Biharamuro  mkoani Kagera katika ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Mhe. Bashe amesema mbali na Serikali kutoa mbegu bure kwa Wakulima pia amewahakikishia Wananchi wa Biharamulo soko la uhakika la mazao ya Pamba, Kahawa na Tumbaku.

Amesema Wakulima watauza zao la Pamba kupitia Chama Kikuu cha Ushirika cha Chato na MBCU na Kuelekeza Bei elekezi ya zao hilo la Pamba kuwa  kati ya  Shilingi, 1560 mpaka 1900.

Waziri Bashe amewaambia Wakulima hakutokuwa na makato ya Aina yoyote pia Serikali imefuta tozo ya zao la Kahawa na Mkulima atauza kahawa bila makato yoyote.

"Wakulima wa Robusta Mhe. Rais hapa walikua wanakatwa tozo 47 Hadi tozo ya viburudisho Kiongozi wa Ushirika akiingia ofisini Mkulima anakatwa shilingi mbili kwaajili ya kiongozi kukaa kwenye kiti ofisini, Mhe Rais tumefuta tozo."

Aidha ameongeza kuwa Serikali imejipanga kutatua tatizo la mafuta ya kula nchini kwa kutoa mbegu za Alizeti bure katika Wilaya ya Biharamulo ili Wakulima waanze kulima kwa wingi zao hilo.

Mhe. Bashe amebainisha kuwa katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imetenga fedha kwaajili ya Miradi ya Umwagiliaji, na Wilaya ya Biharamulo ina mradi wenye hekta Takribani 3000 wa umwagiliaji unakwenda kutekelezwa na mwezi Julai Mwaka huu Serikali itatangaza mradi wenye hekta 1500.