Skip to main content
Habari na Matukio

Zambi: Wahujumu wa Ushirika Kukiona

Naibu Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika Mheshimiwa Godfrey Zambi amesema serikali itachukua hatua kali kwa watu wote watakaohusika na kuhujumu vyama vya ushirika hapa nchini. 

Mheshimiwa Zambi aliyasema hayo wakati akitoa salamu zake katika ziara ya Waziri wa Kilimo Chakula na Ushrika Mheshimiwa Eng. Christopher Chiza mkoani Morogoro.

“Viongozi wa vyama vya ushirika ndio tatizo Kubra katika ustawi wa ushirika hapa nchini kwani wamekuwa chanzo cha kuhujumu ushirika” aliongeza Mhe. Zambi.

Wamekuwa wakitumia nafasi zao za uongozi kwa kujipendelea katika utoaji wa mikopo,  alisisitiza Mheshimiwa Zambi katika hotuba yake.

“Tumetunga sheria namba 6 ya Ushirika ya mwaka 2013 itakayowabana viongozi hawa wa ushirika wanaokwenda kinyume na uendeshaji wa ushirika” alifahamisha Mheshimiwa Zambi.

Sheria hii ni kali sana na itawabana kikamilifu wanaohujumu ushirika  na hivyo kurudisha nyuma nia ya wananchi kuwa na maisha bora, aliongeza.

Alisema  tatizo lingine linalokwamisha na kuathiri ushirika ni utitiri wa vyama vya ushirika katika sehemu moja.

Kuna vyama vya ushirika ambavyo havifanyi kazi iapasavyo katika kuendeleza ushirika wetu bali vinakuwepo kwa jina tu.

“Kuna umuhimu  kuwa na vyama vichache vyenye ufanisi kuliko ilivyo sasa ambapo kuna mlundikano vyama usio na tija kwa wanaushirika” alifahamisha Mhemiwa Zambi.