Skip to main content
Habari na Matukio

ZAWADI KUTOLEWA KWA KATA ITAKAYOFANYA VIZURI KATIKA KILIMO - BASHE

Na Bashiri Salum, Wizara ya Kilimo

Chato

 Wizara ya Kilimo imeandaa mpango maalum wa kutoa zawadi  kwa Kata itakayofanya  vizuri katika  uzalishaji wa mazao nchini kwa kuzingatia kanuni bora za Kilimo

Kauli hiyo imetolewa jana (02.10.2019) na Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe alipofanya ziara ya kukagua mwenendo wa Kilimo cha pamba wilayani Chato mkoa wa Geita.

Bashe alisema Watendaji wa Kata na Vijiji wanalo jukumu la kuhamasisha na kusimamia kilimo  na masoko ya mazao ili mpango huu wa utoaji zawadi ufanikiwe .

“Wizara itapanga utaratibu wa zawadi hizo mara baada ya  fomu maalumu ambayo itatumika kukusanya taarifa mbalimbali za wakulima kukamilika.” alisema Naibu Waziri

Alibainisha kuwa zawadi zitaanza kutolewa msimu ujao 2019/2020 wa kilimo kulingana na  taarifa zitakazopatikana kwenye kata zote nchini

"Kama wizara tunataka maafisa kilimo ngazi ya wilaya kuhakikisha kata itakayofanya vizuri itapewa zawadi kutokana na vijiji vyake kuzalisha mazao kwa wingi na ubora utakaokidhi mahitaji ya soko la ndani na nje ” alisema Bashe.

Alisema kamati maalumu zitaundwa katika ngazi ya Halmashauri kuandaa vigezo vya kupata washindi kulingana na aina ya mazao katika kata husika.

 Bashe amesema mfumo huo utasaidia upatikanaji wa taarifa muhimu  na mawasiliano ya moja kwa moja na mkulima hivyo kuondoa tatizo la ukosefu wa taarifa

Ili kufikia malengo ya nchi kuongeza uzalishaji,Naibu Waziri Bashe ameziagiza  Halmashauri zote nchini kuweka malengo ya uzalishaji wa mazao kwa kila  kata sambamba na ujenzi wa maghala ya kuhifadhia mazao ya wakulima.

Kwa upande wake Afisa Kilimo Umwagiliaji na Ushirika Wilaya Chato, Salimu Msuya amemueleza Naibu Waziri kwamba uzalishaji umekuwa ukipungua maeneo mengi ,kutokana na wakulima wengi kutofuata kanuni bora za kilimo (best agriculture practices)  

 Msuya alisema wilaya ya Chato itaendelea kutoa elimu ya kilimo bora na chenye kuzingatia teknolojia ili wakulima wapate tija ya uzalishaji na kuongeza uhakika wa soko hivyo kukuza kipato cha kaya.

Mwisho