Skip to main content
News and Events

CHAMA KIKUU CHA USHIRIKA NYANZA CHATAKIWA KUJITEGEMEA KIMAPATO-KUSAYA

Mwanza.

Wizara ya Kilimo imekiagiza Chama Kikuu cha Ushirika mkoani Mwanza (Nyanza) kubuni njia muafaka za kujitegemea kiundeshaji kwa kutumia rasilimali nyingi ilizonazo.

Agizo hilo limetolewa leo(30.04.2020) Jijini Mwanza na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya wakati alipofanya kikao na watumishi wa chama hicho na kuelezea kusikitishwa kwake na hali ya utendaji wa chama hicho kushindwa kujiendesha.

“ Tunataka kuona sasa Nyanza mnakuwa na utendaji unaolenga kujiendesha kibiashara tofauti na ilivyokuwa zamani ili wakulima wa pamba wanufaike na ushirika  kupitia mali zao” alisema Kusaya

Alibainisha kuwa wizara ya Kilimo ina lengo la kuiona Nyanza inasimama yenyewe na ya kisasa inayojiendesha kibiashara kuwakomboa wakulima wa pamba.

Kusaya alisema Chama Kikuu cha Nyanza kinazo mali nyingi ikiwemo nyumba,maghala na mashamba ambayo kwa sasa hazitumiki kuzalisha mali kwa faida na kuwa zingine bado zinamilikwa isivyo halali na baadhi ya watu na kutaka ripoti ya mali hizo ipelekwe wizarani kwake ifikiapo Mei 15 mwaka huu.

“ Watieni moyo wana ushirika ili wawe na imani na Nyanza.Nataka nione mkijitegemea na kuwa leo nilitegemea kusika ripoti ya mafanikio badala ya kunieleza matatizo ya madeni” alisema

Aidha aliagiza kuwa agizo la Waziria Mkuu kuhusu urejeshwaji wa nyumba nane (8) zilizokuwa zikimilikiwa isivyo na watu binafsi litekelezwa kwa nyumba hizo kuwa na hati miliki za umma .

Kwa uande wake Kaimu Meneja Mkuu wa Nyanza Martha Ndeto alisema tayari nyumba saba(7) zilizokuwa zikimilikiwa kinyume ya utaratibu zimerejeshwa na hati zake zipo kwa Msajili wa Ardhi na kuwa kazi inaendelea kufuatilia moja iliyobaki.

Ndeto aliongeza kusema Nyanza kwa sasa inakabiliwa na madeni makubwa yanayofikia shilingi Bilioni 4.23 toka wa mabenki,taasisi za serikali na wafanyabiashara.

Katika hatua nyingine Katibu mkuu Kusaya alitembelea Bodi ya Pamba yenye makao makuu yake jijini Mwanza na kuagiza kuwa waongeze malengo ya uzalishaji pamba kutoka tani 450,000 za sasa hadi tani 700,000 mwaka ujao .

Alisema amesikitishwa kuona viwanda vya kuchambua pamba kwenye mikoa ya Shinyanga,Simiyu na Mwanza vinashindwa kufanya kazi mwaka mzima kutokana na upungufu wa malighafi.

“ Nia yangu nikiwa Mtendaji Mkuu wa Wizara ya Kilimo ni kuona uzalishaji wa pamba unaongezeka ili viwanda vipate malighafi ya kutosha na wakulima wapate fedha za kutosha “ alisisitiza Katibu Mkuu huyo

Mkurugezi Mkuu wa Bodi ya Pamba Tanzania Marco Mtunga alisema bodi yake inaendelea na mikakati ya kuongeza uzalishaji pamba na kukutafuta  pembejeo za kutosha ili wakulima wapate mavuno bora mengi na soko la uhakika.

Katibu Mkuu Kusaya yupo katika ziara ya kikazi mikoa ya Kanda ya Ziwa kukagua maandalizi ya msimu wa ununuzi wa pamba utakaonza hivi karibuni na kuongeza na watumishi wa taasisi zilizo chini ya Wizara yake .

Mwisho

Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Wizara ya Kilimo

MWANZA

30.04.2020I