Skip to main content
News and Events

HAKUNA UTHIBITISHO WA UWEPO NZIGE NCHINI –MHE. HASUNGA

Dodoma.

Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga amebainisha kuwa kwa sasa hakuna tatizo la nzige hatarishi kwa mazao ya wakulima nchini.

Alitoa kauli hiyo ya serikali jana (29.01.2020) ofisini kwake Dodoma wakati alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu tishio la uwepo wa nzige wa Jangwani na kusisitiza kuwa hakuna taarifa za uthibisho wa uwepo wa wadudu hao waharibifu wa mazao.

Hasunga alisema kuwa nchi ipo salama na visumbufu vya mazao na mimea na mazao ya kilimo vinaendelea kudhibitiwa na wataalam wa kilimo mara vikijitokeza.

“Hadi sasa, hakuna uthibitisho wa kitaalam kuhusu uwepo wa Nzige wa Jangwani hapa nchini” alisema Hasunga

Serikali imeendelea kuchukua hatua kukabiliana na milipuko hivyokila mwaka hutenga fedha kukabiliana na milipuko ya visumbufu vya mazao na mimea vinavyoweza kujitokeza alisisitiza Waziri huyo wa kilimo nchini.

Alibainisha kuwa tayari hatua za kuratibu upatikanaji wa viuatilifu maalum vya kudhibiti Nzige na kwa sasa kuna jumla ya lita 7,000 kwa ajili ya tahadhari zipo nchini.

Katika kuhakikisha taarifa za viashiria vya nzige zinapatikana mapema Waziri Hasunga alisema tayari wataalam wa wizara wapo katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Mara ambayo inapakana na nchi jirani ya Kenya kufuatiliaji na kubaini viashiria vya uwepo wa Nzige wa Jangwani.

Waziri wa Kilimo ametoa wito kwa wabia wa maendeleo, taasisi mbalimbali za umma na sekta binafsi kushirikiana na Wizara yake kutekeleza mpango wa kukabiliana na tishio la Nzige ili kuhakikisha kwamba nchi inaendelea kuwa na uhakika wa chakula na kipato kwa wakulima

Mwisho.