Skip to main content
News and Events

HALMASHAURI ZIANZISHE VITALU VYA MBEGU ZA MKONGE - MAJALIWA

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameziagiza Halmashauri zote zinazolima zao la mkonge kuanzisha vitalu vya kuzalisha miche bora ya mkonge na kuigawa kwa wakulima ili kufufua mashamba zaidi na kuongeza uzalishaji zao la mkonge nchini.

Ametoa agizo hilo leo (20.01.2021) wakati alipozindua rasmi zoezi la ugawaji miche bora ya mkonge iliyozalishwa katika kituo cha Utafiti wa zao la mkonge (TARI) Mlingano wilaya ya Muheza mkoa wa Tanga.

Majaliwa alisema mkakati wa serikali ya awamu ya tano ni kuhakikisha wakulima wadogo na wakubwa wakifufua mashamba yao ya mkonge hali itakayokuza uzalishaji wa zao hilo muhimu nchini.

“Kila halmashauri ambapo zao la mkonge linastawi ianzishe vitalu vya kuzalisha mbegu bora za mkonge kwa kuwa na mashamba ekari kumi ifikapo mwezi Aprili mwaka huu “ alisema Majaliwa.

Waziri Mkuu alisema ni jukumu la Maafisa Kilimo na Ugani kwenye halmashauri kuanza kukusanya vikonyo vya mkonge toka kwenye mashamba yaliyozeeka na kutumia kuzalisha miche mipya na bora kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Mlingano iliyo na jukumu la kukuza uzalishaji wa mbegu za mkonge.

Awali Waziri Mkuu alipokea taarifa ya uzalishaji miche bora ya mkonge toka kwa Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti Mlingano Dkt. Catherine Senkoro kuwa tayari imezalisha miche milioni 2.4 ya mkonge kwa njia ya vikonyo na kuigawa kwa wakulima.

Dkt. Senkoro aliongeza kusema TARI Mlingano imefanikiwa kupanda hekta 31(sawa na ekari) kati ya 65 za miche bora ya mkonge zitakazogawiwa kwa wakulima mwaka huu .

“Miche hii ipo tayari shambani na kuanzia mwezi Septemba mwaka huu tutaanza kuigawa kwa wakulima kwenye mikoa yote inayolima zao hilo nchini” alisema Dkt. Senkoro na kuwa TARI inazalisha mbegu kwa njia ya vikonyo na maabara (tissue culture).

TARI Mlingano ina uwezo wa kuzalisha miche 120,000 ya mkonge kwa njia ya maabara na miche zaidi ya 500,00 kwa njia ya vikonyo ambapo changamoto ni upanuzi wa maabara ili izalishe zaidi miche bora.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe alisema wizara yake imejipanga kuhakikisha mikoa mingi zaidi inalima zao la mkonge ili kuongeza uzalishaji toka tani 36,298 za sasa hadi tani 120,000 ifikapo mwaka 2025.

Kwa mwaka 2020 uzalishaji wa jumla wa mashamba ya wakulima wadogo ilikuwa tani 9,729.39 sawa na asilimia 27%. Uzalishaji kwenye mashamba matano ya Bodi ni tani  4,806.76 sawa na asilimia 13.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Bashe alisema ili kuongeza kasi ya uzalishaji na ufufuaji mashamba ya mkonge nchini ,wizara imepanga kuwa suala la uagiza magunia nje ya nchi linafikia ukomo kwa bodi za mazao zote kutakiwa kutumia magunia ya katani yanayozalishwa nchini.

“Wizara itahakikisha kama nchi tunapunguza uagizaji wa Magunia ya Katani kutoka nje ya nchi. Kwa kuanzia katika zao la Korosho msimu huu wakati wakutangaza Tender(zabuni) ya vifungashio tumeeleza kwamba tunatoa priority( kipaumbele) kwa vivungashio vya katani” alisema Bashe

Akitoa taarifa kwenye kikao cha wadau wa mkonge Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge Saad Kambona alimweleza Waziri Mkuu kuwa tayari maagizo ya serikali yameanza kutekelezwa ambapo nyumba 21 kati ya 32 zilizokuwa zimeporwa au kumilikiwa kinyume cha utaratibu zimerejeshwa Serikalini.

Kambona aliongeza kusema Bodi hiyo sasa imeanza kufanya kazi vema ambapo katika mwaka 2019/2020 ilifanikiwa kukusanya zaidi ya Shilingi milioni 344 toka vyanzo mbalimbali hatua iliyowezesha ianze kujitegemea kimapato .

“Tumefanikiwa kuanza kukusanya mapato kutoka vyanzo vyetu vilivyokuwa havifanyi kazi ambapo tumeweza kukusanya Shilingi milioni 344 mwaka jana na kuiwezesha Bodi kutoa gawio kwa serikali Shilingi milioni 10 “ alisema Kambona.

Zao la Monge Tanzania hulimwa zaidi katika Mikoa ya Tanga, Morogoro, Arusha, Mwanza, Shinyanga na Kilimanjaro.

Waziri Mkuu yupo mkoani Tanga kwa ziara ya kikazi ya siku tatu kuhamasisha kilimo cha mkonge nchini.

Mwisho.

Imeandaliwa na;

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Wizara ya Kilimo

TANGA

20.01.2021.