Skip to main content
News and Events

MIRADI 11 YA ERPP MOROGORO YAKAMILIKA KWA ASILIMIA 97-KUSAYA

Wizara ya Kilimo imefanikiwa kupitia mradi wa kuongeza tija na uzalishaji wa zao la mpunga (ERPP) imefanikiwa kukamilisha miradi kumi na moja iliyopo mkoani Morogoro na itakabidhiwa kwa wakulima mwisho wa mwezi huu.

Hayo yamebainishwa leo (15.01.2021) na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya wakati alipoongea na wakulima wa kijiji cha Msolwa Ujamaa Halmashauri ya Mji wa Ifakara Morogoro wakati alipokagua utekelezaji wa mradi(Expanding Rice Production Project-ERPP) wa ujenzi wa ghala la kuhifadhia mazao na skimu ya umwagiliaji .

Kusaya alisema ameridhishwa na hatua ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa maghala matano yalipo kwenye wilaya za Mvomero, Kilombero na Kilosa kufuatia wakandarasi wake kukamilisha kazi kwa asilimia 99.

“Mradi wa ERPP ulilenga kujenga maghala matano, skimu za umwagiliaji tano na maabara moja ya kilimo kwenye wilaya za Mvomero, Kilombero na Kilosa ambapo wizara inatarajia kukabidhi miradi hiyo kwa wakulima ifikapo mwisho wa mwezi huu.Nimefarijika kuona miradi yote ipo tayari isipokuwa mmoja wa skimu ya Kilangali wilaya ya Kilosa uliofikia asilimia 77chini ya mkandarasi Lukolo Construction Ltd. ” alisisitiza Kusaya.

Katibu Mkuu huyo aliyefanya ziara ya kukagua miradi ya ujenzi wa maghala ya kuhifadhia mazao ya Kigugu (Mvomero), Msolwa Ujamaa (Ifakara) pia skimu za umwagiliaji za Kigugu (Mvomero),Kilangali (Kilosa) na Msolwa Ujamaa (Ifakara) kwa nyakati tofauti.

Kusaya alitoa wito kwa wakulima mkoa wa Morogoro ambao mradi wa ERPP umetekelezwa kuitunza miradi hii iliyogharimu fedha nyingi za serikali iliidumu na kunufaisha vizazi vijavyo.

“Miradi yote hii kumi na moja ni zawadi iliyotolewa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa wakulima wa mkoa wa Morogoro iliwaongezea uhakika wa upatikanaji wa chakula na kipato cha kaya ,hivyo wizara ya kilimo itapenda kuona ikitumika kuchangia kukuza uchumi wa wakulima wa zao la mpunga” alisema Kusaya.

Kwa upande wake Mratibu wa Mradi wa Kuongeza Tija na Uzalishaji wa Zao la Mpunga (ERPP) Mhandisi January Kayumbe alisema mradi huo uliotekelezwa kwa miaka mitano ulianza mwaka 2016 kwa upande wa Tanzania Bara na Zanzibar.

Mhandisi Kayumbe alisema mradi wa ERPP ulikuwa na malengo manne,kwanza kupeleka mbegu bora zampunga kwa wakulima zilizofanyiwa utafiti ambapo walifanikiwa kupatambegu 13  kupitia mashamba darasa ambapo baada ya utafiti wakulima wengi walichagua mbegu aina ya SARO 5 iliyotoa mavuno mengi.

Litaja lengo la pili la mradi ilikuwa ni kuboresha skimu za umwagiliaji katika wilaya tatu za Mvomero,Kilosa na Kilombero ambapo jumla ya skimu tano zimejengwa tayari na tatu mradi umefanikiwa kujenga maghala matano ya kuhifadhia nafaka kwenye wilaya hizo tatu.

Mhandisi Kayumbe aliongeza kusema anaishukuru serikali ya Awamu ya Tano kwa kushirikana na Benki ya Dunia kwa kutoa fedha Dola za Kimarekani Milioni 22 ( milioni 16.9 Bara na milioni 6.4 Zanzibar) zilizofanikisha kukamilisha mradi huu wa mfano kwenye sekta ya umwagiliaji nchini.

“ Mradi umekamilika kwa asilimi 97 na wizara yetu ya Kilimo imepanga ifikapo tarehe 31 mwezi huu itakabidhi miradi yote hii 11 kwa wakulima na wananchi wa mkoa wa Morogoro.

Kuhusu tija kwenye uzalishaji wa mpunga Mhandisi Kayumbe alisema mradi umefanikiwa kuongeza uzalishaji wa mpunga toka tani 2 kwa hekata mwaka 2016 hadi tani 5 kwa hekta mwaka 2019 na baadhi ya wakulima mmoja mmoja wa lifikia tani 10 kwa hekta ndani ya kipindi cha miaka mitano ya utekelezaji wa mradi huu wa ERPP mkoani Morogoro.

“ Mradi umefanikiwa kufanya wakulima wa Morogoro kuwa na uhakika wa chakula kwa familia na sasa ziada inatumika kuuza kwenye masoko na kuwapatia kipacho cha uhakika “ alisema Mhandisi  Kayumbe.

Mhandisi Kayumbe alitaja changamoto ya mvua nyingi katika miaka miwili iliyopita kuwa ilikwamisha mradi kukamilika kwa wakati hivyo kupelekea kuongezwa kwa miezi tisa kufikia mwezi huu .

Naye Mwenyekiti wa skimu ya umwagiliaji kijiji cha Msolwa Ujamaa  Asumini Mwinyi alitoa pongezi kwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa uongozi wake unaojali wakulima hata kutoa fedha kugharimia mradi huo.

Mwenyekiti huyo alitoa ombi kwa Wizara ya Kilimo kabla ya kukabidhi mradi huo isaidie kuondoa kasoro ndogondogo kama maeneo ya vivuko na kukarabati barabara ya kwenda mashambani iliyoharibiwa wakati wa utekelezaji wa mradi.

Naye msimamizi wa mradi wa ujenzi wa skimu ya Msolwa Ujamaa Abdulamid Mbaga alisema wamekamilisha ujenzi wa mfereji mkuu wenye urefu wa kilometa 2.5  pamoja na mifereji ya pili yenye urefu wa kilometa 7.5 hivyo kuyafikia mashamba ya wakulima wengi.

Mbaga aliongeza kusema kwa sasa wanakamilisha marekebisho madogo hususan ujenzi wa matuta kuongeza udongo,ujenzi wa vivuko,eneo la kupumzikia wakulima na vyoo vya shambani kabla hawajakabidhi mradi .

MWISHO

Imeandaliwa na:

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Wizara ya Kilimo

IFAKARA

15.01.2021