MTAALA MPYA WA KILIMO WAZINDULIWA

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Mhandisi Mathew  Mtigumwe  leo tarehe 21 Machi, 2019 amezindua rasmi mtaala wa Kilimo uliohuishwa  baada ya ule wa zamani uliofahamika kama mtaala wa kilimo mseto kuboreshwa.

Akihutubia mamia ya wataalamu kutoka Taasisi mbalimbali za Umma na Binafsi katika mkutano uliofanyika kwenye Hoteli ya Morena  iliyopo Jiji la Dodoma, Mhandisi Mtigumwe amesema Mtaala huo ni matokeo ya  mahitaji ya soko la ajira (Labour Market Need Assessment) yaliyofanywa na wataalamu waelekezi toka Chuo Kikuu Cha Iringa na kubaini umuhimu kwa jamii.

Aidha  Katibu Mkuu huyo amebainisha kwamba kulingana na maendeleo ya teknolojia kumekuwa na mahitaji makubwa ya wanafunzi wa Vyuo vya Kilimo kuwezeshwa kubobea katika fani au taaluma zao (field of specialization) hivyo mtaala huo umekuja wakati muafaka.

Aidha Mtaala  huo umehuishwa na kuingiza taaluma na moduli mpya katika nyanja za Ushirika katika Kilimo, Hisabati katika Kilimo, Mawasiliano, Mabadiliko ya tabianchi, Jinsia na Kilimo Endelevu; ili kuwajengea uwezo na umahiri wahitimu katika sekta ya Kilimo (Agriculture Production).

“Napenda kuwajulisha kuwa mtaala huu umezingatia kanuni za NACTE, hivyo ninayo furaha kusema kuwa tumefanikiwa kupata sio tu Mtaala Uliohuishwa bali pia ni Mtaala wenye moduli mpya sita zilizojaza nafasi ya moduli za Mifugo” alisistiza Mhandisi Methew Mtigumwe

 Hata hivyo Mhandisi Mathew Mtigumwe alibainisha kwamba  Mtaala mpya wa  Kilimo (Agriculture Production) umehusisha  moduli mpya zilizoingizwa katika tuzo ya taifa ya ufundi daraja la nne  NTA Level 4: mbinu za msingi za mawasiliano Basic Communication Skills na hisabati katika kilimo Basic Mathematics in Agriculture; tuzo ya taifa ya ufundi daraja la tano NTA Level 5: menejimenti ya mazingira Environment Menagement na Kanuni bora za Ushirika katika kilimo Principles of Cooperatives in Agriculture; na tuzo ya taifa ya ufundi daraja la sita NTA Level 6: kilimo hai/endelevu Organic Farming  na jinsia katika kilimo Gender in Agriculture.

Mtaala uliohuishwa unalenga kutoa wagani tarajali wenye umahiri katika uzalishaji mazao kwa tija na hivyo kuchangia katika sera ya uchumi wa viwanda alisisitiza Mhandisi Mtigumwe.

Awali Katibu Mkuu huyo alishukuru Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Shirika la LWR, Shirika la Kilimo Endelevu Tanzania (SAT), Baraza la Taifa la Elimu ya ufundi NACTE, Wakala wa uzalishaji na usambazaji wa mbegu za kilimo (ASA), Taasis ya Udhibiti wa Ubora wa Mbegu Tanznia (TOSCI), Halmashauri za Wilaya, Makampuni Binafsi, Chuo Kikuu Cha Ushirika Moshi, Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam  na Wizara ya Kilimo  kwa kufanikisha upatikanaji wa mtaala huo.

Aidha, Wakufunzi wetu wanahitaji kupata mbinu bora katika kutekeleza Mtaala mpya, mazingira rafiki ya kujifunzia na kufundishia; haya ni maeneo mengine ya mashirikiano, nasi tuko tayari kushirikiana na wadau mliopo na wadau wengine alimalizia Mhandisi Mtigumwe.

MWISHO