KATIBU MKUU KILIMO AKABIDHIWA RASMI OFISI

Mhandisi Mathew Mtigumwe aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo leo, (tarehe 24 Machi 2020) amemkabidhi rasmi ofisi Katibu Mkuu mpya Bwana Gerald Musabila Kusaya katika halfa fupi iliyofanyika kwenye ofisi za Wizara, Mji wa Serikali Mtumba, Jijini Dodoma.

Akiongea katika hafla hiyo, aliyekuwa Katibu Mkuu, Mhandisi Mtigumwe amesema kwa muda wa miaka mitatu ya utumishi wake katika Wizara ya Kilimo ameshirikiana na watumishi na kufanikiwa kuleta mabadiliko makubwa kwenye eneo la uanzishaji wa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II), mchakato wa uanzishwaji wa Sheria ya Kilimo, uanzishwaji wa Sheria ya Maendeleo ya Ushirika, maboresho ya Sheria ya Tume ya Umwagiliaji, pamoja na mchakato wa uanzishwaji wa Mamlaka ya Maendeleo ya Mazao ambayo itaziunganisha Bodi saba za Mazao.

Mhandisi Mtigumwe aliwasihi watumishi kutoa ushirikiano kwa Katibu Mkuu mpya kuendelea kushirikiana na Wakuu wa Idara na Vitengo ili yakamilike kwa wakati.

“Katibu Mkuu (Mhe. Gerald Kusaya) naomba endelea kushirikiana na timu hii ya Menejimenti ni imani yangu kuwa baada ya kukamilika kwa kazi hii, utendaji wenu utakuwa rahisi na Wizara itafanikiwa katika maeneo mbalimbali” Alisisitiza Mhandisi Mtigumwe.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa nyaraka mbalimbali za Wizara, Katibu Mkuu Kusaya amemshukuru Mhandisi Mtigumwe kwa kuhudumu katika nafasi hiyo na kuongeza kuwa mabadiliko mengi aliyoyafanya, yatamsaidia katika utendaji wake wa kazi za kila siku.

Kusaya amesema wizara yake itaendelea kutekeleza kwa weledi malengo yote waliyowekewa na Serikali ikiwemo kuhakikisha nchi inakuwa na uhakika wa chakula.

 “Mhandisi Mtigumwe, hapa ni nyumbani kwako, na niseme tu kuwa bado unakaribishwa kutupa ushauri, sisi bado tutaendelea kushirikiana na wewe na kwa kuzingatia unyeti wa Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo, ina mahusiano makubwa na Sekta ya Kilimo”. Katibu Mkuu mpya wa Wizara ya Kilimo.

Mhandisi Mathew Mtigumwe amehamishiwa Ofisi ya Waziri Mkuu ambako atapangiwa majukumu mengine.