Skip to main content
News and Events

Serikali imeombwa kuwasaidia wasindikaji wa korosho

Washiriki wa Mkutano wa tatu wa Kimataifa wa korosho waliiomba Serikali kutoa msaada kwa wasindikaji wa korosho katika kufikia malengo.

Ombi hilo lilitolewa katika mkutano huo  uliofanyika katika Hotel ya Serena Jijini, Dar es Salaam.

Mkutano huo ni wa Kimataifa uliwakutanisha wadau wa zao la korosho kutoka nchi za Bara la Afrika, Ulaya na Asia.

Suala la Serikali kuwa na juhudi ya makusudi katika kuwasaidia wasindikaji wadogo na wa kati lilikuwa ni kilio cha wachangiaji mada walioshiriki mkutano huo.

Mchangiaji wa kwanza kupaza sauti yake alikuwa ni Waziri wa zamani katika Serikali ya Awamu ya Tatu, Bwana Maokola Majogo ambaye ni Mjumbe wa Bodi ya Korosho, Mkulima na Msindikaji ambaye alisema kuwa kazi ya kuongeza thamani ya mazao katika Bara la Afrika ni ghali na kama wakulima wadogo na wa kati wakiachiwa kazi hiyo peke yao bila ya msaada wa Serikali ni dhahiri kuwa hawataweza, kuleta maendeleo ya zao la korosho.

Bwana Majogo aliongeza kuwa, ili mafanikio ya kweli yaweze kupatikana na kuonekana katika sekta ndogo ya korosho ni vyema maandalizi yaanze katika hatua ya uzalishaji (shambani) na hatmae usindikaji.

Bwana Majogo alikaririwa akisema “Hakuna namna ya kupata matokeo chanya; ni vyema uwekezaji ukaanzia kwenye maarifa ya uzalishaji na baadae kuwapatia wakulima, kipaumbele cha kuwasaidia fedha za mikopo nafuu ambayo, itawasaidia kununua mashine za kubangua, kupanga madaraja na kufungasha ili kuongeza thamani ya zao la korosho.”

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Bwana Mfaume Juma ambaye katika mkutano huo aliwasilisha mada inayohusu maendeleo ya sekta ndogo ya korosho nchini, alisema njia moja ya kuongeza uzalishaji katika zao la korosho ni kuhamasisha uwekezaji kwenye ujenzi wa viwanda vidogo na vya kati vya usindikaji wa mazao ya korosho.