Waziri wa Kilimo Mhe. Charles Tizeba amesema serikali imeruhusu wafanyabiashara na wakulima kuuza nje ya nchi mahindi ili kuimarisha soko na kuchangamsha bei ya zao hilo.
Akiongea ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivi karibuni Mhe. Dkt.Tizeba amesema serikali imeamua kuwaruhusu wafanya biashara kupeleka nje ya nchi ili kuwasaidia wakuliama kupata soko lenye manufaa na kuogeza kipato ili waweze kuandaa msimu mwingine.
Dkt Tizeba amesema Serikali imefikia hatua hiyo baada ya kufanya utafiti na kubaini kuwa mahindi yaliopo kwa wakulima ni mengi na bei ya mahindi hapa nchini ni ndogo sana.
“Wapo wakulima wana mahindi lakini wanashindwa kuuza kwa kuwa bei ni ndogo hivyo kushindwa kuingia kwenye msimu wa kilimo kwa kukosa pesa za kununua pembejeo”.
Aidha DKT. Tizeba Amewaambia wabunge na watanzania kwa ujumla kwamba awali Kamati ya Kilimo ilikutana na kujadili suala la mahindi kutokana na unyeti wake, ambapo matokeo yake Serikali kupitia Wakala wa hifadhi ya chakula (NFRA) ilianza kununua mahindi kwa wakulima .
Wakala wa hifadhi ya chakula (NFRA) walianza kununua mahindi katika sehemu zenye uzalishaji mkubwa katika Mikoa ya Njombe na Ruvuma na baadae Rukwa na Songwe ili kuwawezesha wakulima kuingia katika msimu mwingine wa kilimo alisisitiza Dkt. Tizeba.
Aidha amewataka wakuu wa Mikoa na Wilaya kuacha kuzuia mahindi kutoka nje ya Mikoa yao au Mkoa moja kwenda mwengine ili kuwasaidia watanzania wengine wenye mahitaji hayo.