SERIKALI YATAJA MKAKATI WA KUDHIBITI MAGONJWA YA ZAO LA MIPAPAI.

Na.MathiasCanal,Wizara ya Kilimo.Dodoma.

Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imefanya utafiti na kugundua kuwa ugonjwa wa Ubwiliunga ndio unaoathiri mipapai kwa kiwango kikubwa.
Baada ya kugundulika ugonjwa huo, Wizara ya Kilimo imechukua hatua za kuudhibiti kwa kutumia viuatilifu vyenye viambata vya croripynfos (udhibiti wa kwenye udongo), Profenophos na Dichlorovosch (udhibiti kwenye majani). 

Aidha, njia nyingine ya uthibiti ni kwa kutumia mbinu bora za kilimo (Cultural Control) kwa kupanda miche wakati wa kiangazi ili mimea isishambuliwe ikiwa michanga, kupalilia shamba kwa wakati na kung’olea miche iliyoathirika na utumiaji wa wadudu marafiki (BiologicalControl) .

Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba ameyasema hayo leo (5 Novemba 2019)  bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mheshimiwa Zainabu Mussa Bakari aliyetaka kufahamu serikali imechukua hatua gani kudhibiti maradhi katika mimea ya mipapai nchini ambayo yanahatarisha kupotea kwa mimea hiyo.

Amesema kuwa Serikali inaendelea kutoa elimu kwa wakulima kuhusu kufuata kanuni bora za kilimo ili kuepuka magonjwa mbalimbali yanayoweza kuathiri mimea ukiwemo mpapai.
Serikali kupitia Kituo cha Utafiti cha TARI (Horti) Tengeru imeendelea kufanya utafiti wa magonjwa na wadudu wanaoathiri mazao ya bustani ikiwemo mipapai.

Utafiti huo umegundua kuwa ugonjwa wa Ubwiliunga unaoathiri mipapai unasababishwa na vimelea vya kuvu (fungus) vijulikanavyo kitaalam kama Oidiumcaricae papaya.
Amewahaikikishia wakulima, kuwa Mipapai haiwezi kupotea nchini kwa kuwa tayari njia za kudhibiti  magonjwa na wadudu wanaoshambulia mimea hiyo zipo.

Aidha,Naibu Waziri Mgumba amesema Wizara itaendelea kuwaelimisha wakulima na wadau mbalimbali juu ya udhibiti wa ugonjwa na wadudu wanashambulia mimea na mazao ikiwemo mipapai ili kuongeza uzalishaji na tija.

Mwisho