Skip to main content
News and Events

Tunajiandaa kuja na Sheria ya Kilimo kwa ajili ya kumtetea Mkulima – Waziri Hasunga

waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) amesema ipo haja ya kuanzishwa kwa Sheria ya Kilimo itakayotoa suluhisho la changamoto zinazamkabili Mkulima na Sekta hiyo kwa ujumla.

 

Waziri Hasunga ameyasema hayo leo tarehe 11 Februari 2019 wakati wa kikao cha siku mbili baina yake na Watafiti wa kilimo kutoka Taasisi mbalimbali za kilimo nchini.

 

“Kuna kila sababu ya kuanzishwa haraka sheria ya kilimo, kwa sababu hatuna Sheria ya Kilimo na inayotumika sasa ni Sera ya Kilimo, iliyotungwa mwaka 2013 ambayo pia inahitaji kupitiwa upya” amesema

 

Mhe. Hasunga ameongeza kuwa Sheria zinazotumika kwa sasa ni za Bodi za Mazao mbalimbali, ambazo pia zinachangamoto zake na kuna mazao ambayo hayana Bodi kiasi kwamba kuwatetea Wakulima wa mazao hayo inakuwa vigumu.

 

Mazao yaliyo katika utaratibu wa Bodi ni pamoja na zao la Pamba, Kahawa, Chai, Korosho, Pareto na Tumbaku kwa upande wa mazao ya biashara, mazao ambayo hayana bodi ni yale ya chakula ambayo nayo yana mchango mkubwa katika uchumi wa Taifa.

 

Waziri Hasunga amewataka Watafiti hao kutumia kikao hicho kutoa michango yenye tija, nini kifanyike katika Sekta ya Kilimo kwakuwa Watafiti wana wigo mpana wa kuitoa Sekta hiyo kutoka sehemu moja hadi nyingine.

 

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Omary Mgumba alisema kikao hicho ni cha kipekee kwakuwa kimewakutanisha Wataifiti na Wataalamu kutoka Taasisi za utafiti na watafiti wakufunzi wabobevu kutoka vyuo vya kilimo nchini.

 

“Ni furaha kuwaona leo hii kwa wingi wenu, eneo kubwa la kutiliwa mkazo ni katika suala la masoko, tunafanya tafiti nyingi kuhusu mbegu bora lakini hatuna tafiti za kutosha kuhusu masoko ya mazao ya kilimo,” Alikaririwa Naibu waziri wa Kilimo Mhe Innocent Bashungwa

 

Mtafiti kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo Naliendele Dkt. Fortunus Kapinga alisema kikao hicho kimekuja wakati muafaka ambapo utafiti wenye tija na wenye kuzingatia wakati unahitajika zaidi ili kutatua changamoto za kilimo nchini.

 

“Kazi yetu Watafiti nikuhakikisha utafiti wa kina unafanyika ili kuondoa changamoto za wakulima, naamini tutabadilishana uzoefu lakini pia tutaishauri serikali kuangazia katika tafiti zaidi na kutujengea uwezo ili tuzalishe tafiti zenye tija na uzalishaji bora,

”alisema

 

Kikao kama hicho kitaendelea kesho Tarehe 12 Februari 2019 baina ya wizara na wadau wa kilimo wa sekta binafsi na baadaye kikao kama hicho kitafanyika pamoja na wadau wa maendeleo ya kilimo wakimataifa na waliopo nchini.

 

Baada ya vikao hivyo Wizara na wadau wote wataamua muda gani sera ya kilimo ipitiwe upya na kuanzishwa mchakato wa muswada wa sheria ya kilimo na hatimaye kupata sheria ya kilimo.