Skip to main content
News and Events

Vituo vya Utafiti , Mafunzo na Ugani washauriwa Kushirikiana

Vituo vya Utafiti  wa Kilimo, Vyuo  vya Mafunzo  pamoja na huduma za Ugani washauriwa kuimarisha ushirikiano  katika utendaji wa shughuli zao ili kuleta maendeleo ya kilimo.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mafunzo Dkt. Wilhelm Leornad Mafuru akiongea na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini ofisini  kwake hivi karibuni anasema Vituo vya Utafiti na  Vyuo vya Mafunzo ya kilimo  vimejengwa kimkakati ili kuweza kushirikiana na kuleta matokeo chanya katika sekta hiyo.

Dkt. Mafuru amesema kuwa  watafiti wanaibua maarifa na ujuzi mbalimbali ambao ni buni utumiwe na wakufunzi katika utoaji wa  mafunzo  kwa  maafisa ugani, hivyo kama utaratibu huo utatiliwa mkazo mchango wa taasisi hizo katika maendeleo ya sekta ya kilimo utakuwa mkubwa.

Hata hivyo Wakuu wa vyuo  wamekumbushwa kuwa wabunifu, wenye  mioyo ya  kujituma na wazalendo katika kusimamia mali za umma ili kuendeleza lengo la uwepo wa Vyuo hivyo.

Aidha katika kuboresha Vyuo vya Kilimo Dkt. Mafuru anasema kwa sasa Idara imejipanga kuhamisha wakufunzi kutoka vyuo vyenye ziada ya wakufunzi na kuwapeleka katika vyuo vyenye upungufu.

Utekelezaji wa Mradi wa kuendeleza Sekta ya kilimo awamu ya pili (ASDP II) umelenga kuboresha vyuo vya mafunzo ya kilimo kwa kurabati miundombinu, kuvipatia vifaa vya kufundishia na kujifunzia, vifaa vya usafiri, kujenga uwezo wa wakufunzi kwa mafunzo ya muda mrefu na mfupi, kuhuisha mitaala iendane na wakati, kuanzisha na kuboresha mashamba darasa kwaajili ya mafunzo kwa vitendo alisema Dkt. Mafuru.