Skip to main content
News and Events

WAFANYABIASHARA WANAOPANDISHA BEI YA SUKARI KIHOLELA HATUTAWAVUMILIA- HASUNGA

SERIKALI imeweka wazi bei ya  sukari nchini ambapo bei ya rejareja haitazidi Sh 2600 kwa mikoa ya karibu kama Dar es Salaam na Sh 3200 kwa mikoa ya mbali kama Katavi.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga leo jijini Dodoma wakati akitoa bei hizo , amesema bei hizo zimezingatia umbali wa kila eneo katika mikoa yote nchini.


Akizungumza na waaandishi wa habari, Hasunga amesema serikali imefikia hatua hiyo baada ya kubaini kuwa wafanyabiashara wa sukari wamepandisha bei kiholela kinyume na utaratibu huku akitoa onyo kali kwa ambaye atakaidi bei iliyotolewa.


" Tunawatangazia wafanyabiashara wote wenye tabia ya kupandisha bei kiholela kuacha mara moja kwani serikali haipo tayari kuona wananchi wake wanaumia kwa manufaa ya watu wachache"ameeleza Hasunga.


Hasunga amesisitiza kuwa watachukua hatua kali kwa mfanyabiashara ambaye atabainika kujinufaisha kwa kuuza sukari bei ya juu kuliko ya kawaida ya soko.
Hasunga ameongeza kuwa mfanyabiashara atakaekiuka maagizo hayo atakua ametenda kosa na hivyo kufikishwa katika vyombo vya sheria ili apate adhabu ambayo itahusisha kumnyang'anya leseni ya biashara au kulipa faini au adhabu zote kwa pamoja.


Aidha Hasunga ameongeza kuwa wafanyabiashara hao walidhani kutokana na viwanda vingi kushindwa kuzalisha sukari ya kutosha na uwepo wa ugonjwa wa Corona sukari ya kuziba pengo haitopatikana kirahisi hivyo wakaanza kujinufaisha wao kwanza.


Naye Waziri wa Biashara na Viwanda, Innocent Bashungwa ametoa onyo pia kwa wafanyabiashara ambao watapandisha bei ya sukari huku akiiagiza tume ya ushindani FCC kushirikiana na Bodi ya Sukari kupanga bei ya jumla ya sukari.


" Serikali haitomvumilia yoyote ambaye atakaidi agizo la bei ya maelekezo lililotolewa, kwa wafanyabiashara wote wanapaswa kuteleleza agizo hili kwani limezingatia vigezo na gharama zote ambazo wanazitumia," Amesema Bashungwa.


Bei za sukari ni kama ifuatavyo, Iringa (2900), Mbeya (3,000), Rukwa, Katavi, Ruvuma (3,200), Njombe (2,900), Lindi, Mtwara (2,800), Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Tanga (2,700), Dar (2,600), Pwani, Morogoro (2,700), Kagera, Mwanza, Shinyanga,Simiyu, Geita (2,900), Mara (3,000), Kigoma (3,200), Singida, Tabora, Dodoma (2,900), Songwe (3,000).


MWISHO