Skip to main content
News and Events

WAKULIMA WA TARIME KUPATA MBEGU NA MBOLEA KWA BEI ELEKEZI YA SERIKALI-KUSAYA

Wizara ya Kilimo imesema itahakikisha wakulima wa wilaya ya Tarime na mkoa wote wa  Mara wanapata mbegu bora za mahindi na mbolea kwa bei elekezi ya serikali ili kudhibiti biashara ya magendo mpakani.

Kauli hiyo ya serikali imetolewa leo (21.11.2020) na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya alipozungumza na wakulima na wananchi wa kijiji cha Nyamwaga wilaya ya Tarime wakati alipokagua mashamba darasa ya kahawa,mihogo na migomba.

Kusaya alisema hayo kufuatia malalamiko ya wakulima wa Tarime kusema hawapati mbegu bora za mahindi na mbolea zinazozalishwa nchini hali inayowafanya wategemee bidhaa hizo toka nchini Kenya zinazoingizwa kinyemelea mpakani Sirari.

Akizungumzia suala la uhaba wa mbegu na mbolea Mkuu wa Wilaya ya Tarime Mhandisi Mtemi Msafiri alimweleza Katibu Mkuu huyo kuwa wakulima wanapata shida ya kupata pembejeo za serikali na kuwa Tarime hazifiki hali inayowafanya wakulima kushindwa kuzalisha kwa tija mazao hususan mahindi yanayotegemewa kwa chakula.

“Tuna shida kubwa ya mbegu bora za mahindi hapa Tarime na zinazopatikana zinauzwa bei kubwa mfano kilo mbili kwa shilingi 15,000 na nyingi zinatoka nje ya nchi “alisema Mhandisi Msafiri

Katibu Mkuu Kusaya aliwahakikishia wakulima hao kuwa wizara yake kupitia Wakala wa Mbegu (ASA) na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA) utafikisha mbegu za mahindi na alizeti pia mbolea mkoani humo mapema kabla ya Desemba mwaka huu .

“Nimeagiza Mtendaji Mkuu wa ASA Dkt. Sophia Kashenge afike hapa Mara na ahakikishe mbegu bora za mahindi zinauzwa kwa bei elekezi ya serikali ili wakulima wengi wamudu na kutoendelea kuumizwa na wafanyabiashara. Mbegu hizi zitauzwa chini ya shilingi 10,000 “alisema Kusaya hatua iliyopokelewa kwa shangwe na wakulima.

Kusaya aliongeza kuwaeleza wakulima hao kuwa tayari ameelekeza mbolea iletwe mapema kabla ya Desemba na Malmaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA) na kuwa iwafikie wakulima kwa bei elekezi ya serikali.

“Niwasihi wakulima wangu muwe na subira kabla ya Desemba mwaka huu TFRA wataleta mbolea hapa Tarime na mkoa wote wa Mara itakayouzwa kwa bei elekezi “alisisitiza Kusaya.

Akiwa kijijini Nyamwaga kwenye mkutano wa hadhara wakulima walieleza kuwa wanauziwa mbolea aina ya NPK mfuko wa kilo 50 kwa bei ya Shilingi 60,000 hadi 80,000 kwa inayotoka Kenya na ya Tanzania kwa Shilingi 80,000 hadi 100,000 hivyo kushindwa kumudu.

Katika hatua nyingine Kusaya aliwashauri wakulima wa wilaya ya Tarime pamoja na kulima mazao ya chakula wajikite pia kuzalisha mazao ya kahawa, chai na migomba yanayostawi vema kutokana na hali ya hewa nzuri na kuwa wizara yake itatoa utaalam na pembejeo ikiwemo mbegu bora.

Kusaya aliongeza kuwahakikishia wakulima wa migomba na mihogo kuwa tatizo la wadudu wasumbufu litapatiwa suluhisho mapema kupitia taasisi ya Utafiti wa kilimo (TARI) ambapo watafiti watafika Tarime na Butiama kukutana na maafisa ugani na wakulima

“Niwatoe hofu wakulima wa mihogo na migomba kuhusu tatizo la ugonjwa unaoharibu mazao hayo, kuwa wiki ijayo wataalam toka TARI Maruku (Bukoba) na wale wa TARI Ukirigulu (Mwanza) watafika hapa Tarime kutatua changamoto za magonjwa haya kwa kuwafundisha maafisa ugani namna ya kukabiliana na wadudu hawa” aliahidi Katibu Mkuu Kusaya.

Ili kuhakikisha wakulima wanapata elimu na teknolojia ya kuwasadia kutatua changamoto za kilimo, Katibu Mkuu huyo wa kilimo alitoa agizo kwa wakurugenzi wa halmashauri nchini kuacha kuwatumia maafisa ugani kwenye kazi za utawala ikiwemo kazi ya utendaji wa vijiji na kata.

“Hawa maafisa ugani wameajiliwa kwenda shambani hivyo wasipangiwe kukaimu utendaji wa vijiji au kat. Tunataka kila kijiji kiwe na afisa ugani kuwasaidia wakulima kutatua changamoto za mazao yao” alisema Kusaya.

Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Kilimo amehitimisha ziara yake ya siku tatu mkoani Mara kwa kutembelea wilaya za Musoma, Butiama na Tarime ambapo amekutana na kufanya mazungumzo na wakulima pamoja na kukagua shughuli za kilimo mashambani.

Mwisho

Imeandaliwa na;

Kitengo Cha Mawasiliano Serikalini

Wizara ya Kilimo

TARIME

21.11.2020