Skip to main content
News and Events

WAZIRI WA KILIMO MHE JAPHET HASUNGA AFUNGUA SEMINA YA BIMA KWA MAJANGA YA KILIMO JIJINI DAR ES SALAA

Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga (Mb) leo tarehe 7 Februari 2019 amefungua semina ya siku mbili ya Bima kwa majanga ya kilimo nayofanyika kwa siku mbili katika Ukumbi wa BOT Jijini Dar es salaam

 

Akizungumza katika semina hiyo Mhe Hasunga amesema kuwa hiyo ni hatua nzuri katika kuhuisha utoaji wa huduma bora za bima za kilimo kwa kuzingatia matakwa ya Sheria ya Bima ya Mwaka 2009, Sheria na Mipango Mbalimbali katika sekta ya kilimo; kwa kutafutia ufumbuzi wa pamoja changamoto zinazokabili sekta ya kilimo na wakulima nchini.


 

Waziri Hasunga ameupongeza uongozi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Shughuli za Bima Nchini (TIRA) kwa kuandaa mkutano huo muhimu wa wadau wa bima katika kilimo kwani utakuwa na fursa ya kujadili na kuchambua namna ya kuboresha tija kwa wakulima kwa kuwaingiza katika Bima ya Mazao.


 

Alisema kuwa jitihada hizo za sekta ya bima nchini ni kuunga mkono mipango ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe Dkt John Pombe Joseph Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuhakikisha uchumi wa viwanda unafikiwa kwani Viwanda ni Kilimo, na kilimo bora chenye tija hukingwa na bima.

 

Amesema kuwa semina hiyo ikiongozwa na dhima inayosema “Bima za Kilimo Nchini Tanzania: Nafasi na Wajibu katika Utekelezaji” inalenga kuleta majibu katika changamoto ambazo serikali imejikita katika kukabiliana nazo hususani kwa wakulima kote nchini.

 

Aliwataka Wataalamu wa Bima waliohudhuria katika semina hiyo kutambua kuwa sekta ya bima ni kichocheo muhimu katika uchumi wa viwanda na Kilimo chenye tija. Kwa kukinga majanga mbalimbali katika Mnyororo mzima wa sekta ya kilimo kwa sehemu kubwa kuimarisha viwanda.

 

Waziri hasunga amewataka wataalamu katika sekta ya bima na wa upande wa Sekta ya Kilimo kujiuliza na kujibu maswali ya Kwanini mwamko wa wananchi katika bima hususani Bima za kilimo upo chini? (kwa mujibu wa takwimu ni 15% tu ya watanzania hupata huduma za bima) kiwango hicho ni kidogo ikilinganishwa na zaidi ya 75% ya wanojihusisha na kilimo.

 

Ni lini na kwa namna gani wakulima na wafugaji wadogo wa Tanzania wataanza kunufaika na bima za Mazao na Mifugo?, na Njia zipi zitumike kuhakikisha kuwa huduma za bima za kilimo zinakuwa nafuu na zenye tija katika Sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi.

 

Mengine, Ni njia zipi zinaweza kutumika kuwahamasisha Wakulima, Wafugaji na Wavuvi kutumia huduma za bima katika kazi zao na Ni jinsi gani Teknolojia ya Habari na Mawasiliano inaweza kutumika katika kurahisisha upatikanaji wa huduma za bima za Kilimo, Mifugo na Uvuvi.

 

Pia, amehimiza kuelekea lengo la kuhakikisha angalau asilimia 50 ya watu wazima wanapata huduma ya bima ya chini ifikapo mwaka 2028, kutafakari jinsi Tanzania inavyoweza kuimarisha teknolojia zinazojitokeza kama vile majukwaa ya biashara ya digitali na mifumo ya malipo ya simu kutoa huduma za bima na huduma kwa wakulima wanaofikia milioni 38. Ubunifu na ushirikiano katika kupata masoko mapya hususani ya kilimo, mifugo na uvuvi kwa kutumia njia mbadala vitaimarisha ubia kati ya sekta ya kilimo na bima.

 

Awali, Kamishna wa Bima Tanzania Dkt Baghayo Saqware alisema kuwa wazo kuu la kuandaa mkutano huo ni kuendeleza kwa dhati ushirikiano kati ya Taasisi za Umma, Makampuni Binafsi na Mashirika ya Kijamii ili kutoa huduma ya Bima ya kilimo katika jamii kwa wigo mpana.

 

Alisema kuwa kuanzia mwaka 2016/2017 serikali ilizindua mpango wa miaka mitano uliojikita katika kuifanya Tanzania iwe nchi ya uchumi wa kati kwa kutegemea viwanda.

 

Aliongeza kuwa maeneo muhimu ambayo sekta ya Bima (Binafsi) na Taasisi za umma zinaweza kufanya kazi kwa pamoja ili kuongeza ufanisi katika shughuli za Bima ya kilimo kwa kuwa na sera ya Taifa ya Bima, Kuwa na taarifa za wakulima (Data Base), vilevile wananchi kuwa na imani (Kuamini) biashara na huduma za Bima.

 

Zingine ni kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma na wigo wa huduma za Bima nchini, Teknolojia rahisi na rafiki kwa ajili ya kusambaza Bima, kuuza Bima, Kulipa mafao/Madai ya Bima, kusikiliza maoni na mahitaji ya wananchi, na kuchakata maombi ya Bima.

 

MWISHO.