Skip to main content
News and Events

WAZIRI WA KILIMO PROF. ADOLF MKENDA APOKELEWA RASMI WIZARANI NA KUSEMA ATAANZA NA ZAO LA NGANO KAMA

WAZIRI WA KILIMO PROF. ADOLF MKENDA APOKELEWA RASMI WIZARANI NA KUSEMA ATAANZA NA ZAO LA NGANO KAMA AJENDA YA KITAIFA

Waziri wa Kilimo Mhe. Prof. Adolf Mkenda leo mchana tarehe 21 Desemba, 2020 amepokelewa rasmi Wizara ya Kilimo katika Ofisi za Wizara hiyo katika Mji wa Serikali Mtumba na kutoa wito kwa Menejimenti ya Wizara pamoja na Wakuu wa Taasisi kufikia kuongeza tija kwenye Sekta ya Kilimo Mazao hususan zao la ngano na mazao mengine ya biashara.

Waziri wa Kilimo Prof. Mkenda ambaye aliambatana na Msaidizi wake; Naibu Waziri Kilimo Mhe. Hussein Bashe wote kwa pamoja leo wamepokelewa rasmi na Watumishi wa Wizara ya Kilimo katika ofisi za Wizara Jijini Dodoma na wote kwa pamoja wamesisitiza na kuomba ushirikiano ili kuifaya Wizara ya Kilimo kuongeza tija kwenye mazao ya kilimo.

Katika hafla hiyo ya mapokezi. Mawaziri wote kwa pamoja walipata nafasi ya kuongea na Menejimenti ya Wizara ambapo Waziri Mkenda amesema Wizara inajukumu kubwa la kuhakikisha taifa linaendelea kujitosheleza kwa chakula pamoja na kufanya Sekta ya Kilimo Mazao inachangia mara dufu katika pato la taifa.

Waziri Mkenda ameongeza kuwa tija kwenye kilimo bado ipo chini na kuongeza kuwa mazao yanachangia asilimia 18 ya pato la taifa wakati Sekta ya Kilimo kwa ujumla inachangia takribani asilimia 28.2 ya pato la taifa, asilimia 58 ya ajira na asilimia 65.5 ya malighafi inayotumika katika Sekta ya Viwanda, asilimia 28.2 ya pato la taifa na asilimia 30 ya mapato ya fedha za kigeni.

“Ukiangalia zaidi ya asilimia 65 ya Watanzania wameajiriwa kwenye Sekta ya Kilimo; Jambo hili ni lazima tulifanyie kazi kwa ukaribu na kuleta mapinduzi ya kweli. Nchi zilizoendelea unakuta asilimia tano tu (5%) ndiyo wameajiliwa kwenye Sekta ya Kilimo. Ukiangalia hizo takwimu maana yake ni kuwa kwet Tanzania, tija ipo chini. Unatakiwa kuwa na idadi ndogo Wakulima na Watanzania wengine wajikite kwenye Sekta nyingine za uzalishaji”. Amesisitiza Waziri Mkenda.

Waziri Mkenda ameongeza kuwa tija kwenye mazao mengine bado ipo chini na kwamba kila sababu ya kufanya mapinduzi ili kuondokana na hali hiyo.

“Ukiangalia kwenye zao la chikichi kwa mfano; Michikichi mingi inatupa tani 1.6 za ujazo wa mafuta katika hekta moja lakini kwa wenzetu wa Malaysia, Indonesia na Costarica ni tani 10 za ujazo wa mafuta kwenye hekta moja.”

“Tumedhamiria kuondokana na hali hii; Wataalamu wetu kwa kutumia mbegu zetu za ndani wametafiti na kupata mbegu bora ambazo zitaanza kutupa tani tano za ujazo wa mafuta katika hekta moja.”

“Vilevile tukienda kwenye zao la ngano; Mhe. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ametupa maelekezo ya kuachana na utegemezi, tija ipo chini. Uzalishaji kwetu ni tani 1.2 za uzito kwa hekta huku wenzetu Afrika ambao tunashindana nao (Misri) wao uzalishaji ni tani 5.5 kwa hekta.” Amekaririwa Waziri Mkenda.

“Tunahitaji kupambana ili kuondokana na hali. Njia pekee ya kuanzia ni matumizi ya mbegu bora. Pili tutaendelea kutafuta masoko ya uhakika kwa Wakulima wetu na kwenye masoko tutahimiza na kujenga na kuimarisha ushirika. Hapo kabla tulikuwa na Ushirika imara lakini baadae waliingia Viongozi wasio waaminifu walituharibia Ushirika wetu. Tumeanza upya kurejesha Imani kwa Watu kuhusu Ushirika.” Amemalizia Waziri Mkenda.

Naye Naibu Waziri Kilimo Mhe. Hussein Bashe amesema ili Wizara ifikie malengo yalikusudiwa ni vyema Viongozi pamoja na Watumishi wote wa Wizara wakafanya kazi kama timu moja na kuongeza kuwa Watendaji wanapaswa kubadili fikra.

“Nawapongeza kwanza kwa kunipa ushirikiano wa kutosha kabla ya uchaguzi mkuu. Namshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuwa na imani na Mimi na kunirejesha tena. Tuendelee kufanya kazi kwa pamoja na kwa ushirikiano.”

“Jambo la msingi kwetu ni kuimarisha eneo la masoko pamoja na kujenga mazingira mazuri ya kufanya kilimo; Tumeendelea kuzishawishi Benki za biashara kupunguza riba kutoka asilimia 18 hadi hadi asilimia 13 lakini pia tutaendelea kuheshimu maagizo ya Mhe. Rais John Pombe Magufuli.”

“Mhe. Rais amesema sasa kilimo ni biashara na si kilimo cha kujikimu; Tumepanga kuongeza usalishaji kwenye zao ngano na hadi kufikia 2025 walau tuwe tumezalisha tani milioni 1 kwa nchi nzima; Katika kufanikisha jambo hili. Tumeunda timu ya Wataalam kutoka Sekta Binafsi na Serikali kuu. Timu hiyo ina wataalam kutoka Wizara ya Kilimo; Fedha na Mipango pamoja na Viwanda na Biashara.” Amekaririwa Naibu Waziri Bashe.

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya amesema ataendelea kuwa ushirikiano Mawaziri wote ili watekeleze majukumu yao ipasavyo.

“Mimi kama Mtendaji Mkuu ndani ya Wizara. Nitawapa ushirikiano ili mtekeleze majukumu yanu ya kila siku. Mwisho wa siku ni kumsaidia Mkulima mdogo ilia lime kwa tija na faida na bila kusahau; Tutengeneze Mabilionea wengi katika Sekta ya Kilimo.” Amemalizia Katibu Mkuu Kusaya.