Skip to main content
Habari na Matukio

DKT. MPANGO:  HAKUNA TENA NJAA KUPITIA KILIMO CHA UMWAGILIAJI

 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema kuwa kupitia miundombinu ya umwagiliaji inayotekelezwa na Wizara ya Kilimo katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo katika mashamba ya pamoja yaliyo chini ya Programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) itasaidia wakulima kulima kilimo cha umwagiliaji na kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa chakula nchini.

Akizungumza tarehe 22 Agosti, 2024 alipokuwa akizindua Shamba la Pamoja la Dkt. Samia Suluhu Hassan lililopo katika kijiji cha Ndogowe, wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, Mhe. Dkt. Mpango amesema kuwa kupitia skimu ya umwagiliaji wakulima wataweza kuzalisha pasipo kutegemea mvua kwani Mkoa wa Dodoma unautajiri wa maji ya kutosha katika ardhi.

Katika hatua nyingine Mhe. Dkt. Mpango ameitaka Wizara kuweka miundombinu itakayosaidia katika kukabiliana na changamoto ya wanyama waharibifu hususan tembo ambao wamekuwa tatizo katika kijiji hicho ili kuepuka hasara kubwa inayoweza kujitokeza iwapo waanyama hao wataharibu miundombinu.

Wizara pia imetakiwa kuwashirikisha wafugaji katika Shamba la Pamoja la Dkt. Samia Suluhu Hassan ili kuwa na ushirikishwaji utakaoepusha wafugaji kulishia mifugo yao katika shamba.

Mhe. Dkt. Mpango pia ameiagiza Wizara ya Kilimo kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi  katika kufanikisha uanzishwaji wa BBT ya Mifugo ambayo itakuwa na miundombinu wezeshi kwa ufugaji wa wanyama ikiwemo malisho pamoja na maji kwa ajili ya wanyama hao.

Ujenzi wa skimu ya umwagiliaji katika Shamba la Pamoja la Dkt. Samia Suluhu Hassan umegharimu shilingi bilioni 21.7 na hadi sasa utekelezaji wake umefikia 34% ambapo unahusisha ujenzi wa nyumba 8 za pampu, uchimbaji na ufukiaji wa mitaro ya mtando wa bomba za umwagiliaji, ujenzi wa chemba katika maungio ya bomba, n.k.