Skip to main content
Habari na Matukio

KAMATI YA BUNGE YAPONGEZA KITUO CHA VEGETABLE CENTRE

Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo imepongeza kazi kubwa zinazofanywa na Kituo cha World Vegetable Centre kilichopo jijini Arusha, tarehe 3 Julai 2024 kupitia miradi mbalimbali inayobuniwa na kuwafikia wakulima nchini.

Akizungumza kwa niaba ya Kamati, Mhe. Mariamu Ditopile Mzuzuri (Mb) amesema “tumepata fursa kuona wananchi na wakulima wadogo wadogo ambao wametembelea hapa na namna gani kituo kinafikisha shughuli na elimu wanayotoa kwa wakulima ambao wapo maeneo mbalimbali ndani ya nchi yetu.”

“Kituo hiki kinafanya utafiti, mbegu wanazozalisha lazima ziende zikazalishwe zaidi hivyo tunaisihi na kuiagiza Serikali iende sasa ikaone namna gani inaunganisha wazalishaji wa mbegu na kituo hiki,,” ameongeza Mhe. Mariamu Ditopile Mzuzuri (Mb).

Pamoja na mambo mengine, Kamati hiyo pia imetembelea Maabara, Benki ya Uhifadhi wa Vinasaba vya Mbegu (Africa’s Vegetable GenBank) pamoja na mashamba darasa.

Naye Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde (Mhe) amesema Wizara inahamasisha wakulima kulima kilimo cha mazao ya mbogamboga na matunda kwa kuwa ni cha muda mfupi na huingiza fedha nyingi sana za kigeni kuliko mazao mengine yoyote.

Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo hicha cha World Vegetable Centre, Dkt. Gabriel Rugalema amesema kwa mwaka 2024 kituo hicho kimeweza kuwafikia wakulima 504, wanafunzi 120 pamoja na watu kutoka Inchi za nje zaidi ya 600.

Dkt. Gabriel Rugalema ameeleza kuwa wamejipanga kukipanua kituo hicho ndani na nje ya Afrika ili kuwa kituo mahiri na nguli Afrika katika tafiti uendelezaji na uhamasishaji wa mazao ya mbogamboga ambapo mpaka sasa zaidi ya miradi minne inatekelezwa katika kituo hicho.