KATIBU MKUU MWELI AFUNGUA MAONESHO YA TEKNOLOJIA ZA UHIFADHI
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli amefungua Maonesho ya Siku Mbili ya Teknolojia za Uhifadhi na Uongezaji Thamani ya Mazao ya Kilimo baada ya mavuno, yaliyoandaliwa na Asasi Kilele ya Sekta Binafsi (TAHA) chini ya Mradi wa Feed the Future Tanzania yakilenga kuwakutanisha pamoja wadau mbalimbali katika minyororo ya thamani ya mazao ya horticulture na nafaka.
Maonesho hayo yamefunguliwa tarehe 23 Septemba 2024, katika viwanja vya Makumbusho ya Taifa (Mnara wa Mwenge - Arusha) ambapo Katibu Mkuu Mweli ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeongeza bajeti ya kilimo ili kuleta mapinduzi makubwa kwa wakulima ikiwemo kuboresha mazingira wezeshi kwa wakulima kupata teknolojia na masoko ya mazao yao.
Maonesho hayo yameshirikisha wadau mbalimbali kutoka katika minyororo ya thamani ya mazao ya horticulture na nafaka. Wakulima walipata fursa ya kujionea teknolojia za uvunaji, uhifadhi, usindikaji, uongezaji thamani wa mazao, na vifungashio vya kisasa, vyote vikilenga kuboresha ubora na kuongeza thamani ya mazao yao.
Wadau walihamasishwa kuchangia mawazo na teknolojia zinazoweza kusaidia katika kilimo endelevu, huku wakijadili mbinu bora za kuvutia masoko na kuongeza mapato kwa wakulima.
Aidha, Mtendaji Mkuu wa TAHA, Dkt. Jacqueline Mkindi, amemshukuru Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli na Serikali kwa ujumla kaa kuendelea kushirikiana na Sekta Binafsi kwa lengo la kuongeza thamani ya mazao ya kilimo kupitia teknolojia na masoko. Dkt. Mkindi amesema ushirikiano huu ni muhimu katika kuimarisha Sekta ya Kilimo nchini ili wakulima wawe na kilimo chenye tija.
Ameahidi kuwa TAHA itaendelea kutoa ushirikiano wa karibu kwa Serikali ili kuhakikisha malengo ya kuboresha uzalishaji na masoko yanafikiwa. Amesisitiza kuwa kwa pamoja, wanaweza kuleta mabadiliko chanya kwa manufaa mapana ya mkulima na kuimarisha uchumi wa Taifa.