MAONO YA RAIS SAMIA KWENYE KILIMO ITAINUA MAISHA YA WENGI
Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde (Mb) amesema maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwekeza kwenye kilimo cha umwagiliaji ndiyo njia pekee ya kuboresha maisha ya idadi kubwa ya Watanzania. Mhe. Silinde amesema hayo leo tarehe 22 Agosti 2024 alipozungumza kwenye mkutano wa hadhara wa wananchi waliokusanyika kwa ajili ya kumsikiliza Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango katika kijiji cha Mpwayungu, Wilaya ya Chamwino, mkoani Dodoma. Naibu Waziri Silinde amesema Wizara ya Kilimo pamoja na Wananchi wanaojishughulisha na kilimo wanamshukuru sana Rais Mhe. Dkt. Samia kwa juhudi zake za kuwekeza kwenye miundombinu ya umwagiliaji kwani wakulima wataweza kuzalisha katika vipindi vyote vya mwaka pasipo kutegemea mvua. Amefafanua kuwa katika wilaya ya Chamwino pekee Serikali inatekeleza miradi 8 ya umwagiliaji ambayo ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji ambapo imeongeza hamasa kwa wananchi wengi kujishughulisha na shughuli za kilimo.