Skip to main content
Habari na Matukio

MARUFUKU KUONGEZA BEI ELEKEZI YA MBOLEA NCHINI-PROF. MKENDA

 Serikali imesema ni marufuku kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kuongeza bei elekezi ya mbolea bali ihakikishe wakulima wanapata mbolea bora na kwa wakati.

Waziri wa Kilimo Profesa Adolf Mkenda ametoa agizo hilo leo (16.04.2021)  jijini Dodoma wakati alipofungua kikao kazi cha Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania kufuatia maombi yaliyowasilishwa na bodi kwa wizara.

“Bei elekezi ya mbolea sitoongeza licha ya maombi kuletwa wizarani. TFRA nawataka mhakikishe bei ya mbolea iliyopo sasa inaendelea na wakulima wapate mbolea yenye ubora na kwa wakati ili watumie kuzalisha mazao ya Kilimo” alisisitiza Profesa Mkenda.

Profesa Mkenda aliongeza kusema lengo la serikali ya awamu ya sita ni kuona gharama za uzalishaji wa mazao zinashuka ili wakulima waongeze tija kwa kupata mbolea na pembejeo zingine kwa bei rahisi hatua itakayowafanya wakuze kipato chao na uchumi wa nchi kukua.

Ameitaka bodi ya wakurugenzi wa mamlaka ya udhibiti wa mbolea kukutana na wafanyabiashara na wamiliki wa viwanda vya kuzalisha mbolea kujadili na kuweka mikakati ya kufanya wakulima wapate mbolea bora na kwa bei rahisi.

Katika hatua nyingine Prof. Mkenda ameagiza mamlaka hiyo kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) kutoa elimu ya upimaji afya ya udongo kwa wakulima ili watambue aina ya udongo unaofaa kwa aina gani ya mbolea lengo waweze kuongeza tija kwenye uzalishaji  wa mazao.

Waziri huyo wa Kilimo alibainisha kuwa hali ya upatikanaji mbolea nchini umefikia tani 631,660 mwaka huu Februari kati ya mahitaji ya tani 718,051 na kuwa serikali itaendelea kuhamasisha ujenzi wa viwanda vya mbolea hapa nchini ili kupunguza utegemezi wa  mbolea toka nje ya nchi.

Kwa upande wake Veronica Soko mjumbe wa bodi ya TFRA anayewakilisha wakulima wadogo kupitia MVIWATA almeiomba serikali kuweka utaratibu wa kuvikopesha vyama vya ushirika wa wakulima ili wanunue mbolea kwa mfumo wa pamoja hatua itakayosaidia wakulima kupata kwa bei nafua.

Mkulima huyo wa mpunga toka Madibira  wilaya ya Mbarali alibainisha kuwa wanachama wake wamefanikiwa kuongeza uzalishaji wa mpunga kwa njia ya umwagiliaji na matumizi ya mbegu na mbolea bora kuongeza uzalishaji toka gunia 20 hadi 25 kwa hekta hadi kufika tani 7 hadi 10 mwaka 2019.

“Vyama vya ushirika vikitumika kuagiza mbolea kwa mfumo wa pamoja itasaidia wakulima kufikishiwa bidhaa hiyo kwa bei nafuu huku ikiwa iezingatia aina ya zao wanalozalisha  “ alisema Soko.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya TFRA Prof. Anthony Mshandete ameipongeza serikali kwa maelekezo ambayo imekuwa ikiyatoa hatua ianayosaidia bodi yake kuwafikia wakulima wengi kwa kufikisha mbolea inayohitajika kupitia mfumo wa ununuzi wa pamoja( BPS).

Prof. Mshandete amesema bodi hiyo ilioanzishwa  kwa Sheria ya Mbolea Namba 9 ya mwaka 2009 itaendelea kuhakikisha inadhibiti ubora wa mbolea ili wakulima wanufaike  na kuwezesha Kilimo kuchangia zaidi kwenye pato la Taifa .

“Mkakati wetu ni kuhamasisha watanzania wengi waanzishe viwanda vya mbolea hapa nchini hali itakayosaidia kupata mbolea bora na yenye gharama nafuu hivyo kuachana na utegemezi wa mbolea toka nje ya nchi” alihitimisha Prof. Mshandete.

Takwimu za Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania zinaonesha katika mwaka 2020 Tanzania imetumia Dola za Kimarekani Milioni 229.8 kuingiza nchini mbolea tani 659,197 toka nje ya nchi.

Mwisho
Imeandaliwa na ;
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Kilimo