Mbegu Mpya za Mazao Mbalimbali Zaidhinishwa
Kamati ya Taifa ya Mbegu (National Seed Committee) imeidhinisha matumizi ya aina 29 za mbegu mpya za mazao mbalimbali ya kilimo, mazao hayo ni mahindi,mpuga,alizeti karanga na chai.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi Mhe. Mwigulu Nchemba kwa vyombo vya habari, inasema kuidhinishwa kwa aina hizo za mbegu kunafuatiwa mapendekezo yaliyofanywa na kamati ya Taifa ya kupitisha aina mpya ya mbegu za mazao (The National variety Release Committee) katika kikao kilichofanyika kuanzia tarehe 16 – 17 Machi 2016, makao makuu ya Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi Jijini Dar es salaam.
Aidha, aina hizo mpya za mbegu zimefanyiwa utafiti na kugundulika kuwa zinasifa mbalimbali ikiwemo kustahimili ukame,kutoa mavuno mengi,ukinzani dhidi ya magonjwa na wadudu,kukomaa mapema na kupendwa na wakulima.
Mhe. Nchemba aliongeza kuwa utafiti wa kina ulifanywa na vyuo vya utafiti vipatavyo12 na kuweza kuzalisha aina mpya za mbegu hivyo kupatikana aina 16 za mahindi,2 za mpunga, 4 za alizeti, 3 za karanga na 4 za chai.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa aina hizo za mbegu zitaanza kuzalishwa na makampuni mbalimbali ya uzalishaji mbegu pamoja na Wakala wa Taifa wa mbegu za kilimo (Agriculture Seeds Agency-ASA), kwa lengo la kuzifikisha aina hizo mpya za mbegu bora kwa wakulima kuanzia msimu ujao wa kilimo 2017/2018.
“ Hatua hiyo ya kamati inalenga kuongeza tija na kipato kwa mkulima”, iliongeza sehemu ya taarifa hiyo ya Mhe. Nchemba.