TANZANIA KUIUZIA ZAMBIA NANI 650,000 ZA MAHINDI
Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) imeingia makubaliano na nchi ya Zambia kununua tani 650,000 za mahindi kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa Zambia kufuatia ukame unaoikabili nchi hiyo.
Mkataba huo umesainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa NFRA, Dkt. Andrew Komba pamoja na Mratibu wa Maafa Kitaifa nchini Zambia, Dkt. Gabriel Pollen tarehe 29 Juni 2024, jijini Dar es Salaam; na kushuhudiwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb) na Waziri wa Kilimo wa Zambia, Mhe. Reuben Phiri.
Akieleza kuhusu makubaliano hayo, Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe (Mb) amesema mkataba huo utatekelezwa kwa miezi 8 ambapo maghala manne ya NFRA yatahusika kuwezesha mahindi hayo ya tani 650,000. Aidha, Waziri Bashe amesema kuwa Tanzania itanufaika na Dola za Marekani milioni 250 katika manunuzi hayo.
Aidha, Serikali imeingia mkataba mwingine wakuuza tani 500,000 za mahindi katika Serikali ya Jamhuri wa Watu wa Congo, pamoja na mkataba wa kuuza tani 100,000 na Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (World Food Programme - WFP). Mikataba yote hii, pamoja na ule wa Zambia, itakua na jumla ya tani 1,100,000.
NFRA itaanza kununua mahindi tarehe 10 Julai 2024, na sasa imeanza kusaini mikataba ya wauzaji wa Tanzania. Lakini pia Tanzania inaendelea kutekeleza mkataba na WFP wa kuuza unga nchini Malawi. “Niwahakikishe wakulima wote wa mahindi, bei ya NFRA itatangazwa na itakua wazi, NFRA itanunua mahindi kwa zaidi ya shilingi 500/kilo,” ameeleza Mhe. Waziri Bashe.
Amefafanua zaidi kuwa ni muhimu kufahamu kuwa mikataba hii inatekelezwa na NFRA kwa kushirikiana na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB). Hivyo, Waziri Bashe amesema kuwa mauzo ya kwenda Zambia ichukuliwe kama fursa pia kwa wasafirishaji.
Timu ya Tanzania na Zambia zitakaa kwa pamoja kujadili na kupanga taratibu za usafirishaji, kwa lengo la kuyapa makampuni ya Tanzania na Zambia kipaumbele katika kushiriki kikamilifu kwenye fursa hiyo muhimu.