TUTAPAMBANA NA SOKO LA MUHOGO- MKENDA
Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda leo tarehe 7/5/2021 amekutana na wadau wa zao la muhogo ili kujadili fursa za masoko zilizopo katika kukuza uchumi wa nchi na kuongeza kipato kwa mkulima.
Kikao hicho kimefanyika jijini Dodoma katika ukumbi wa Morena kwa kuhudhuriwa na wataalam kutoka Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Mambo ya Nje, Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na TAMISEMI.
Mabalozi walioshiriki kwa njia ya mtandao ni balozi wa China, Uganda, Rwanda na Burundi. Kwa upande wa taasisi za serikali ni pamoja na TARI,TRA,TBS,Ushirika,SIDO,SUA,TANTRADE. Sekta binafsi ni pamoja na TPSF, AGRA, ESRF, Serengeti breweries, CTI na agroforest. Benki ni TADB,NMB,CRDB, Equity bank.
Aidha,Prof. Mkenda amepata fursa ya kuzindua mkakati wa Muhogo na amefurahishwa sana na watafiti wetu ambao wamegundua mbegu mpya na zenye ubora zaidi. Kauli hii aliitoa baada ya kunukuu hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan alipohutubia Bunge la Tanzania kwa kuzungumzia sana kuhusu kilimo,mifugo na uvuvi hasa utafiti.
Prof. Mkenda amesema kuwa kwa mbegu ya kawaida hekta 1 mkulima anapata tani 5 mpaka 8 za muhogo. Kupitia taasisi zetu za utafiti TARI Kibaha imefanya utafiti wa mbegu bora za muhogo zinazohimili magonjwa mfano batobato na kupelekea kuongezeka kwa uzalishaji kwa kupata tani 20,30 hadi 50.
“kilimo bila utafiti hatuwezi kufanya chochote,soko la china la muhogo ni kubwa. Hatutaweza kwenda kwa mkulima anayelima bila tija kupata soko” alisema Mkenda
Hata hivyo ameendelea kusema kuwa serikali ikijikita kwenye kilimo bora wakulima wataweza kulima kwa tija na kupata masoko ambapo watakuwa wameinua kipato cha wakulima wadogo wadogo.
Prof. Mkenda ameainisha vipaumbele vya wizara yake kuwa itawekeza kwenye utafiti wa wataalam wa kilimo , kuzalisha mbegu bora zaidi katika mashamba yote 13 ya ASA na kuitaka taasisi hiyo kulima kilimo cha umwagiliaji ili kuongeza uzalishaji wa mbegu, kuwekeza kwenye ugani kwa mikoa 3 ya kielelezo ambapo afisa ugani ataweza kumfundisha mkulima kuhusiana na mbegu bora na pia ameahidi kuipatia mikoa hiyo pikipiki 1500 kama kitendea kazi ili maafisa ugani waweze kuwafikia wakulima kwenye halmashauri zao na kufufua mashamba ya mfano.