Skip to main content
Habari na Matukio

WAKULIMA WA NJOMBE WAISHUKURU NFRA

Wakulima wa mahindi wa mikoa ya Iringa na Njombe wameishukuru Serikali kwa kuwapatia elimu ya uzalishaji wa mahindi yenye ubora jambo linalowawezesha kuuza mahindi yao kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) bila vikwazo.  Wakulima hao wamesema kutokana na ubora wa mahindi yao yamekuwa hayakataliwi  wanapoyafikisha kwenye vituo ya NFRA.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Dkt. Hussein Omar amewapongeza wakulima hao kwa kuzalisha mahindi yenye ubora na kuagiza NFRA kuendelea kutoa elimu ya uzalishaji na utunzaji wa mahindi yenye ubora.  Amesisitiza kuwa mkulima anapouza mahindi yake kwa NFRA alipwe fedha zake ndani ya siku tano. I ngezeko la uzalishaji wa mahindi linatokana na ruzuku ya mbolea iliyotolewa na Serikali.

Naibu Katibu Mkuu Dkt. Omar ameendelea na ziara yake iliyoanza tarehe 29 Agosti 2024 katika mikoa ya Arusha, Manyara, na baadae mikoani Iringa na Njombe tarehe 30 na 31 Agosti 2024 ya kukagua zoezi la ununuzi wa mahindi ya wakulima linalotekelezwa  na NFRA kwa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Ameielekeza NFRA kuwasiliana na wateja wote walionunua mahindi kwa kuchukua shehena ya mahindi waliyoyanunua ili kupisha nafasi ya kuhifadhi mahindi ya wakulima.  Aidha, Dkt. Omar amewaambia wakulima hao kuwa Serikali inanunua mahindi kwa shilingi mia saba kwa lengo la kuwasaidia wakulima  kuuza mahindi kwa faida.

Naibu Katibu Mkuu Dkt. Omar anaendelea na ziara yake ya kukagua vituo vya kununulia mahindi vya NFR na kutatua changamoto zinazojitokeza kwenye vituo hivyo.