Skip to main content
Habari na Matukio

WIZARA YA KILIMO KUTATUA CHANGAMOTO YA “RUMBESA” KWA WAKULIMA WA ZAO LA KITUNGUU

 

Wakulima wa zao la kitunguu katika Kata ya Ilkinding’a, Wilaya ya Arumeru, Mkoani Arusha wametiwa moyo na Wizara ya Kilimo katika kutatua changamoto ya kuuza mazao bila kipimo cha uhakika, almaarufu kama “rumbesa”. 

 

Ahadi hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli wakati wa ziara yake ya kikazi tarehe 23 Septemba 2024 kwenye mashamba ya wakulima hao. 

Amesema kuwa jukumu la Wizara ya Kilimo ni kuwahakikishia wakulima masoko yasiyo na changamoto, hivyo kuongeza uzalishaji na kipato chao.  “Nimekuja shambani kujifunza na kuona hali halisi. Kuna vitu vipo katika ngazi yangu na pia kwa Viongozi wengine, hivyo nitaenda kushirikiana nao ili tuone namna ya kutatua changamoto hii ya rumbesa,” amesema Katibu Mkuu Mweli.

Aidha, Mwenyekiti wa Wakulima wa zao hilo katika kata ya Ilkinding’a, Bw. Danieli Lukuma amesema kuwa wakulima wapatao 1,900 katika eneo hilo wanazalisha vitunguu ndani ya ekari 1,980; ambapo kwa mwaka wanazalisha tani 20,000 ambazo huuzwa katika masoko ya ndani na nje ya nchi. 

 

Hata hivyo, ameeleza kuwa wakulima hao wamejikuta wakilazimika kuuza kwa mfumo wa “rumbesa” kutokana na kutokuwa na sheria za kuwabana wanunuzi.

 

Naye Mtendaji Mkuu wa TAHA, Dkt. Jacqueline Mkindi amesema kuwa “huu ni mwanzo wa utatuzi wa changamoto za wakulima wa zao la kitunguu; hususan kupitia ushirikiano kati ya Serikali na Sekta Binafsi katika kuboresha hali ya wakulima wa mazao ya horticulture kwa ujumla. 

 

Maana ya kuweka “rumbesa” ni kuzidisha ujazo wa mifuko ambayo ni mbinu inayotumiwa katika usafirishaji wa bidhaa, ambapo mfuko unakuzwa ili kuongeza ujazo wa bidhaa ndani yake.  Badala ya kutumia mifuko au kontena ya kawaida, wafanyabiashara au wakulima hu tumia mbinu hiyo kuongeza ujazo wa mifuko ili kuweza kubeba bidhaa nyingi zaidi na kuongeza ujazo kiholela huku kuleta madhara ya bidhaa kuhifadhiwa vibaya, na hivyo kuathiri ubora wa mazao