HOTUBA YA UFUNGUZI WA KONGAMANO LA VIJANA KATIKA KILIMO ILIYOTOLEWA NA MHESHIMIWA JAPHET N. HASUNGA
Mheshimiwa Brigedia Jenerali Nicodemas Mwagela, Mkuu wa Mkoa wa Songwe,
Mheshimiwa Joachim Wangabo, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa,
Mheshimiwa Juma Homera, Mkuu wa Mkoa wa Katavi,
Mheshimiwa Albert Chalamila, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya,
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Songwe,
Katibu Tawala Mkoa wa Songwe,
Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya mliopo,
Wakurugenzi wa Idara, Taasisi za Kiserikali na Sekta Binafsi;
Maafisa Kilimo, Mifugo na Uvuvi mliopo.
Wawakilishi wa Taasisi za Kifedha;
Wataalam mbalimbali mliopo,
Vijana wote mliopo;
Wanahabari;
Mabibi na Mabwana.
Bwana Yesu Asifiwe, Tumsifu Yesu Kristo, Asalaam Aleikhum
Ndugu Washiriki, Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetuwezesha kukutana leo hapa katika tukio hili muhimu tukiwa na afya njema. Nichukue nafasi hii kuwashukuru Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa yote ya Katavi, Mbeya, Katavi na Rukwa wakiongozwa na Mkuuwa Mkoa mwenyeji wa Songwe, Mheshimiwa Brigedia Jenerali Nicodemas Mwagela kwa kushiriki nasi katika Kongamano hili muhimu la vijana. Aidha, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kabisa, kwa vijana, Taasisi za umma, Wawakilishi wa taasisi na mashirika mbalimbali ya sekta binafsi na wawakilishi wa Wizara za Kisekta kwa kukubali mwaliko wetu na hatimaye kuja kushiriki nasi. Vile vile naipongeza Kamati ya Maandalizi ya Kongamano hili kwa kushirikiana na Uongozi wa Mikoa kwa kufanikisha maandalizi na kufanikisha Kongamano.
Ndugu Washiriki, Vijana ni nguvu kazi na rasilimali watu inayotegemewa kwa maendeleo ya taifa lolote duniani. Katika nchi yetu ya Tanzania, vijana ni milioni 16.1 sawa na asilimia 35 ya idadi ya watu wote. Kwa mujibu wa Utafiti wa Nguvu Kazi ya Taifa wa mwaka 2014, nguvu kazi ya vijana ni asilimia 67.1 [G1] ya nguvu kazi yote ya Taifa na kiwango cha ukosefu wa ajira ni asilimia 11.7 ya nguvu kazi yote. Aidha, kwa mujibu wa utafiti huo, asilimia 66.3 ya watu wote walioajiriwa wameajiriwa katika Sekta ya Kilimo. Hivyo, takwimu hizi zinaonesha umuhimu wa Nguvu Kazi ya Vijana na Sekta ya Kilimo kwa maendeleo ya Taifa.
Ndugu Washiriki, Wizara ya Kilimo imeendelea kuwashirikisha wadau mbalimbali wa kilimo katika utekelezaji wa mipango na Programu za Kuendeleza sekta ya kilimo. Baadhi ya wadau ambao Wizara imekutana nao ni wabia wa Maendeleo; Wasindikaji na Wafanyabiashara wa nafaka; Wadau wa Kilimo Hai; Taasisi za Fedha; Watengenezaji, Wauzaji na Wasambazaji wa Pembejeo za Kilimo, Wanajeshi Wastaafu na Wazalishaji wa Mbegu bora. Makundi mengine ni wadau wa mazao ya biashara na mazao mengine kama vile alizeti, zabibu, na parachichi. Mikutano, hiyo inalenga kufahamiana na wadau, kuibua, kutambua na kujadili namna bora ya kutumia fursa zilizopo katika kilimo. Aidha, mikutano hiyo imekuwa ikijadili changamoto mahsusi zilizopo na kuzipatia ufumbuzi.
Ndugu Washiriki, leo hii tumekutana kwa ajili ya Kongamano hili la Vijana ikiwa ni mwendelezo wa utekelezaji wa mipango na Mikakati ya Wizara ya Kilimo ya kukutana na wadau ili kutanzua changamoto zilizopo katika kilimo na kukubaliana namna bora ya kutumia fursa zilizopo. Kwa kutambua umuhimu wa vijana, vijana watafahamishwa fursa za kilimo zilizopo katika Mikoa hii katika mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo. Aidha, katika kongamano hii kutakuwa na mada elimishi zitakazotolewa na wataalam wabobezi wanaoshirikiana na vijana katika kilimo. Mada hizo zitatolewa ili kutupa uzoefu na uelewa mpana ili tuweze kuwa na maamuzi sahihi katika mipango yetu.Vile vile mtapata nafasi ya kusikia simulizi za mafanikio toka kwa vijana waliofaanikiwa katika kilimo. Tafadhali mtumie nafasi hii vizuri kuwasikiliza na mjifunze kikamilifu mbinu walizotumia kufanikiwa kujiajiri na wengie kuajiri vijana wenzao.
Niwasihi washiriki wote, tutumie siku mbili hizi kujadiliana vizuri na hatimaye tutoke na namna tunavyoweza kuzitumia fursa hizo.
Ndugu Washiriki, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo inatekeleza Mkakati wa Miaka Mitano wa Taifa kwa Vijana kushiriki katika sekta ya kilimo (National Strategy for Youth Involvement in Agriculture- NSYIA) wa mwaka 2016/17 hadi 2020/21. Utekelezaji wa Mkakati huo unashirikisha Wizara na Taasisi mbalimbali ikiwemo Wizara za Mifugo na Uvuvi, Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Rais-TAMISEMI. Maeneo Kumi (10) yanazingatiwa katika utekelezaji wa Mkakati huoni pamoja ni yafuatayo:-
i. Kuhakikisha ardhi inayofaa kwa Kilimo imepatikana na kutengwa katika Halmashauri zote nchini kwa ajili ya Vijana kufanya Uwekezaji,
ii. Kuhakikisha upatikanaji wa raslimali za Kifedha umewezeshwa kwa Vijana walio tayari kufanya Uwekezaji katika shughuli za Kilimo,
iii. Kuhakikisha pembejeo, zana za kilimo na huduma zingine za lazima ziwe zimepatikana kwa ajili ya Vijana,
iv. Kuweka miundombinu ya Matumizi ya Umwagiliaji kwa ajili ya Vijana,
v. Kuhakikisha masoko ya uhakika ya bidhaa za kilimo yameboreshwa na kuwezeshwa,
vi. Kuhakikisha maboresho ya kufanya mabadiliko ya Tabianchi yamezingatiwa katika shughuli za kilimo za vijana,
vii. Kuhakikisha kwamba Ujuzi na Mbinu za Ujasiriamali zinahamasishwa kwa Vijana wote nchini,
viii. Kuhakikisha Vijana wanaunganishwa na mikakati mingine ya vijana katika Kilimo,
ix. Kuhamasisha shughuli zenye staha ili kuwavutia vijana wengi kushiriki shughuli za Kilimo,
x. Kuhakikisha Masuala mahsusi ya mtambuka yakiwemo michezo, Jinsia, Mazingira na Ugonjwa wa Virusi vya ukimwi yamezingatiwa katika mipango mbalimbali ya Vijana katika Sekta ya kilimo.
Ndugu Washiriki, kupitia utekelezaji wa mpango huo, mafanikio yameanza kuonekana yakiwemo yaafuatayo:
i. Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kilimo na Chakula (FAO) nchini imekuwa inatekeleza Mkakati Kabambe wa Taifa wa Vijana kushiriki katika Kilimo katika mikoa ya Singida, Dodoma, Morogoro na Pwani. Mradi huo unaotekelezwa kwa kufuata mnyororo wa thamani (Value Chains) unabaini shughuli za vijana, changamoto walizonazo na kuimarisha mahusiano na Halmashauri za mikoa hiyo ili kufanya utekelezaji wa miradi ya vijana kwa pamoja. Aidha, mradi huo umekuwa ukilenga kilimo cha umwagiliaji ili Vijana waweze kuwa na uhakika wa shughuli za kilimo na kuwagawia vifaa vya umwaliaji kama mashine (Irrigation Pumpus). Katika mradi huo, vijana wote katika mikoa hiyo wataweza kufikiwa kadri mikoa na halmashauri itakavyojipanga.
ii. Mradi East Africa Youth Inclusion Program (EAYIP)unaotekelezwa na shirika la Heifer International katika mikoa ya Mbeya, Songwe, Iringa na Njombe na ulizinduliwa mwaka 2017 ukilenga kuwafikia Vijana elfu kumi (10,000) baada ya miaka mitano (5) na leo hii Vijana hao na shirika la Heifer ni miongoni mwa washiriki waliohudhuria hapa pamoja nasi;
iii. Shirika la SUGECO chini ya Chuo Kikuu cha Kilimo (SUA) kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo limekuwa likitekeleza Mkakati wa Taifa wa Vijana kushiriki katika Kilimo (NSYIA) kwa kufundisha Vijana walio nje ya shule na walioitimu ngazi mbalimbali za vyo katika vituo hatamizi vya Morogoro na Mkongo kule wilayani Rufiji katika mkoa wa pwani ili kuwajengea uwezo wa kujifunza kwa vitendo Mpango wa Biashara, Uzalishaji na Ujasiriamali na pia kuwaunganisha na nchi za Israel na Marekani ambazo kwa teknolojia ya kilimo zimepiga hatua kubwa kimaendeleo na kisha wahitimu hao wanaanzisha miradi yao wenyewe na kuajiri Vijana wenzao. Mpaka sasa zaidi ya Vijana 1000 tayari walishamaliza mafunzo hayo na kuajiri wenzao kupitia miradi yao;
iv. Serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania katika kuhakikisha vijana wengi wanashiriki katika kilimo kwa kuzingatia Mkakati wa Vijana wa Taifa, ilielekeza Halmashauri zote nchini kutenga bajeti ya asilimia 10 kwa ajili ya Vijana, wanawake na Wenye Ulemavu katika maeneo yao na utaratibu huo umekuwa ukifanyika katika Halmashauri zilizo nyingi, ambapo asilimia 4 ni kwa Vijana, asilimia 4 kwa Wanawake na asilimia 2 ni kwa wale wenye Ulemavu. Taarifa nilizonazo ni kwamba vijana wengi kupitia vikundi vyao wamekuwa wakinufaika na mkopo huo wa asilimia 10.
v. Serikali kupitia Wizara ya Kazi, Ajira, Vijana na wenye Ulemavu katika ofisi ya Waziri Mkuu imeendelea kutekeleza mkakati wa Taifa wa Vijana kwa kuratibu mfuko wa kuwezesha Vijana kuwekeza ambao mpaka sasa Vikundi zaidi ya 811 nchini vimenufaika na mfuko huo ambao ni miongoni mwa mifuko 19 inayosimamiwa na Baraza la Uwezeshaji wananchi Kiuchumi (NEEC) wakiwemo Vijana.
vi. Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu inatekeleza Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi wa Vijana nchini. Lengo la program ni kukuza ujuzi kwa vijana ili waweze kujiajiri na kuajiri vijana wenzao. Katika kutekeleza azima hiyo, serikali imeamua kutoa mafunzo ya stadi za kazi kwa vijana katika kilimo cha kisasa kwa kutumia teknolojia ya kitalu nyumba (Greenhouse technology). Kwa msingi huo katka mwaka wa fedha 2019/2020 Serikali imejenga jumla ya vitalu nyumba 84 katika halmashauri 81 za mikoa 12 kwa ajili ya kutolea mafunzo ya kilimo cha kisasa kupitia kitalu nyumba ambapo vijana 8,700 wamepewa mafunzo hayo. Ujenzi wa vitalu nyumba na mafunzo katika mikoa 14 iliyosalia hiko katika hatua za maandalizi.
[G2]
Ndugu washiriki, Pamoja na mafanikio hayo yanayoendelea kupatikana kutokana na utekelezaji wa Mkakati huo, Wizara kwa kushirikiana na wadau wakiwemo Shirika la Umoja wa Mataifa la Kilimo na Chakula Duniani (FAO) imeanza kupitia upya mkakati huo ili kuuboresha zaidi uendane na mahitaji ya sasa. Katika hatua za mapitio hayo, vijana watashirikishwa kutoa maoni pamoja na wadau wanaotekeleza miradi mbalimbali kuhusu vijana katika kilimo hapa nchini.
Ndugu washiriki, Kilimo kimeendelea kukua na kutoa mchango kwa uchumi wanchi katika maeneo mbalimbali. Kwa mfano, takwimu zilizopozinaonesha kuwa sekta ya kilimo imechangia asilimia 28.2 ya pato la Taifa ambapo Sekta ndogo ya Kilimo inayojumuisha mazao ya biashara, mazao ya bustani na mazao mengine (nafaka, mikunde na mazao ya mafuta) ilichangia kwa 16.2% ya pato la Taifa kwa mwaka 2018. Aidha, katika kipindi hicho Sekta ya Kilimo imetoa ajira kwa watanzania asilimia 58, imechangia asilimia 30 ya mapato yatokanayo na mauzo ya nje na inachangia kwa asilimia 100 ya mahitaji ya chakula nchini.
Ndugu Washiriki, nichukue fursa hii pia kueleza mboresho ya mifumo, kisera na kitaasisi ambayo Wizara ya Kilimo imeendelea kufanya ili kuoresha kilimo. Baadhi ya maboreshi hayo ni yafuatayo:
i. Kuanzishwa kwa Mfumo wa Ununuzi wa Mbolea wa Pamoja (Bulk Procurement System) ambapo hadi upatikanaji mbole umeongezeka kutoka tani 302,450 mwaka 2015/2016 hadi tani 460,369.2 mwaka 2018/2019. Hadi kufikia Desemba 2019 upatikanaji ulifika tani 400,499 sawa na ongezeko la asilimia 32.4
ii. Kuimarisha Masoko ya Mazao ya Kilimo kupitia Mfumo wa Stakabadhi Ghalani. Kupiia mfumo huu bei ya ufuta imeongezeka kutoka wastani wa shilingi 1,500 mwaka 2005 hadi kufikia shilingi 3,500 kwa kilo mwaka 2019 na kwa upande wa Kakao kwa kipindi hicho bei imeongezeka kutoka shilingi 3,200 hadi shilingi 5,000 kwa kilo.
iii. Kupunguza na kuondoa kodi, ushuru na tozo kero 105 toka 146 zilizokuwa zikitozwa katika mazao ya kilimo,pembejeo na ushirika kati ya mwaka 2015 na 2019.
iv. Kuongeza uwezo wa hifadhi ya mazao kwa kujenga vihenge vya kisasa .Kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) inakamilisha mradi wa ujenzi wa vihenge vyenye uwezo wa kuhifadhi nafaka tani 501,000 toka uwezo wa sasa wa tani 251,000 mwaka 2015.
v. Wizara imeanzisha Daftari la Usajili wa wakulima nchini ambapo hadi sasa jumla ya wakulima1,279,884 wamesajiliwa kwa mazao ya chai, kahawa, pareto, tumbaku, pamba, korosho, mkonge na miwa.
vi. Kuanzisha utekelezaji wa Bima ya Mazao kwa lengo la kuwakinga wakulia na majanga katika kilimo.
Ndugu washiriki, Sasa naomba nizungumzie fursa zilizopo kwenye kilimo hasa kwa vijana ambao ndiyo walengwa wa kongamano hili kama ifuatavyo;-
a) Kwanza kabisa, nchi yetu ina eneo linalofaa kwa kilimo ambalo linakadiriwa kuwa hekta 44 milioni. Kati ya hizo, hekta milioni 29.4 zinafaa kwa kilimo cha umwagiliaji. Eneo hilo, linafaa kwa kilimo cha mazao yote ya biashara na chakula.Nitoe mfano wa mahindi. Mahindi ni chakula kikuu ndani na nje ya nchi yetu. Lakini pia ni chanzo cha chakula cha wanyama na mifugo. Aidha, uzalishaji wa nyama, maziwa, na mayai umekuwa ukitegemea uzalishaji wa zao la mahindi kama chanzo cha moja kwa moja cha chakula cha mifugo. Licha ya kuwa uzalishaji wa mahindi Barani Afrika unafikia tani milioni 50 lakini bado Afrika inatumia zaidi ya dola bilioni 2 kwa ajili ya kuagiza mahindi kutoka nje ya Afrika. Kadri idadi ya watu Afrika inavyozidi kuongezeka na mahitaji ya chakula kama nafaka, yanaongezeka pia. Hii ni fursa nzuri kwa vijana wa Tanzania,kuzalisha kwa wingi ili kufanya biashara ya mazao hasa yanayohitajika kwa wingi ndani nan je ya nchi.
b) Serikali kupitia Wizara ya Nishati, inajitahidi sana kufikisha umeme vijijini ambako ndiko mazo yanapatikana ili kuweza kuyaongezea thamani kwa kuyasindika. Hadi sasa asilimia 70 ya vijiji nchini yaani vijiji 9,000 kati ya 12,2 68 vimepatiwa umeme. Hii pia ni fursa nzuri kwa vijana ya kutumia umeme ilikufanya kazi za kuzalisha na kuchakata mazao ya kilimo,mifugi na uvuvi hivyo kuongeza thamani na uhakika wa soko na bei nzuri.
c) Nchi yetu ina ikolojia tofauti tofauti, hali hii inasababisha baadhi ya maeneo kuwa na mvua za kutosha, na maeneo mengine kuwa na uhaba wa mvua. Maeneo yanayopata mvua za kutosha huzalisha chakula cha kutosha pamoja na ziada. Kwa maeneo ambayo yamezalisha ziada, vijana wanayo fursa nzuri ya kupeleka ziada hiyo kwenye maeneo mengine ambayo hayazalishi vizuri. Hii ni fursa kwa soko la ndani ya nchi. Vilevile, nchi yetu imezungukwa na nchi ambazo hazina fursa kubwa ya kilimo kama tuliyonayo.
d) Fursa katika uvuvi na Mifugo;
a. Uhaba wa upatikanaji wa chakula cha samaki na vifaranga bora kukidhi mahitaji ya soko mfano uzalishaji wa vifaranga nchini ni 21,173,226 ambapo mahitaji halisi ni vifaranga 50,000,000 kwa mwaka. Hivyo kwa kutumia wingi wa mazao ya kilimo vijana mnao uwezo wa kuanzisha viwanda vidogo vya uzalishaji vyakula vya samaki kwani kuna uhitaji mkubwa.
b. Idadi ya mifugo bora ya ng’ombe wamaziwa na nyama ni ndogo sana na hivyo kufanya bidhaa bora za maziwa na nyama kutotosheleza na kusababisha bidhaa hizo kuagizwa nje ya nchi. Kwa upande mwingine, Tanzania imejaliwa kuwa na aina mbali mbali za ng’ombe kama Borani, Mpwapwa na Ankole. Ng’ombe hawa wakiendelezwa wataongeza uzalishaji wa nyama na maziwa yenye ladha nzuri na ya kipekee kutokana na malisho ya asili na matumizi madogo ya madawa kwa kuwa ng’ombe hao wanastahamili magonjwa. Hii itatuongezea hata kupata masoko makubwa ya nyama hususan kwenye hii kanda ya Mashariki naKusini mwa Afrika.Vijana mnayo fursa nzuri kutumia wataalam wetu wa mifugo na uvuvi ili kuanzisha miradi hii ya ufugaji nchini.
[G3]
Ndugu washiriki, zipo changamoto zinazowakabili vijana katika kilimo. Changamoto hizo ndizo zimetufanya tukutane hapa ili tuzijadili na hatimaye kupata suluhisho la pamoja. Miongoni mwa changamoto hizo ni kama ifuatavyo;-
i. Pamoja na serikali kujitahidi kutenga maeneo ya kilimo kwa vijana kupitia Halmashauri kuna baadhi ya Halmashauri hazina maeneo ya kuwatosheleza vijana wanaohitaji kujishughulisha na kilimo. Hali hii inachangia sana vijana wengi kukaa bila kufanyakazi na au kukimbilia mijini na kujihusisha na makundi yasiyo na nia nzuri na hatimaye Taifa kupoteza nguvu kazi kubwa ambayo ingeongeza ustawi wa nchi iwapo vijana hao wangeshiriki katika kilimo.
ii. Kukosekana kwa teknolojia bora na rahisi za kuongeza thamani ya mazao. Matokeo yake bidhaa hizo zinauzwa zikiwa hazijaongezwa thamani au zikiwa chini ya viwango vinavyohitajika kitaifa na kimataifa na hivyo kutokukubalika. Hali hii inaleta umasikini badala ya kupunguza au kuondoa kabisa umasikini, kwa mtu mmoja mmoja na hatimaye Taifa kukosa pato.
iii. Ukosefu wa mitaji toka taasisi za fedha .Hii imechangiwa na masharti magumu na wakati mwingine riba kubwa inayotozwa na taasisi za fedha kwa vijana wanapoenda kukopa.Ili kutatua, katika kongamano hili tumewaalika wadau wa taasisi za fedha kuja kushiriki na kutoa elimu juu ya upatikanaji mikopo kwa urahisi.
iv. Elimu duni ya ujasiliamali katika kilimo, mifugo na uvuvi.Vijana wengi wameonekana licha ya kuwa na elimu ya darasani wanakosa mbinu bora na za kisasa za ufanyaji biashara yenye kuongeza tija.Ni wakati sasa serikali na wadau wa sekta binasfi kusaidia utoajai elimu ya ujasiliamali ili vijana waweze kutumia fursa za uwepo ardhi yenye rutuba,mito na maziwa ,eneo la umwagiliaji na mifugo kubadilisha kuwa fursa ya ajira.
Ndugu washiriki, baadhi ya changamoto nilizozitaja hapo awali, nimezitaja ili iwe chachu ya kuongeza msukumo wa majadiliano katika kongamano hili. Aidha ni matumaini yangu kuwa mada, ushuhudazitakazotolewa na waandaaji, zitawapa nafasi pia ya kuelewa vizuri umuhimu wa vijana kushiriki katika kilimo,mifugo na uvuvi. Majadiliano ya siku mbili yatatoka na maazimio ambayo yatajibu changamoto nilizozitaja hususani fursa zilizopo katika kilimo. Nitoe rai kwa washiriki wote, tusikilize kwa makini, tuwe wawazi, na kwa uhuru tujadili mada hizo kwa mapana na marefu, ili baada ya siku mbili hizi, tutoke na maazimio yatakayojibu changamoto za vijana kushiriki katika kilimo.
Ndugu Washiriki, Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi madhubuti wa Mhe.Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ina nia njema kabisa ya kuhakikisha kuwa tunashirikiana na wadau wote katika kuhakikisha kuwa kilimo kinaendelea na kuondoa changamoto zinazojitokeza. Lakini, Serikali peke yake, haiwezi kuziondoa changamoto hizo bila nyinyi vijana kushirikiana na Serikali yenu.Hivyo, ninawasihi wote, tushirikiane ili tuendeleze nchi yetu kwa moyo wa uzalendo.
Ndugu washiriki, mwisho kabisa, niwashukuru tena kwa kuja kushiriki kongamano hili muhimu. Napenda kuwashukuru na kuwatambua wahisani na wadau waliotuchangia katika kufanikisha maandalizi ya kongamano hili ambao ni Jukwaa la Wadau wa Kilimo (ANSAF), Heifer International SUGECO, JATU,nk
Kipekee napenda sana kuwashukuru wajumbe toka Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe na Halmashauri zote za mkoa wa Songwe kwa kushiriki kikamilifu kwenye maandalizi yaliyofanikisha kongamano hili. Nirejee tena kuwashukuru Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa kwa uongozi bora katika mikoa yenu na ushiriki wenu katika Kongamano hili.
Baada ya kusema hayo, sasa natangaza kuwa “Kongamano letu la kihistoria la kwanza la vijana kushiriki katika kilimo, Limefunguliwa Rasmi”.
ASANTENI KWA KUNISIKILIZA!