HOTUBA YA WAZIRI WA KILIMO MH. JOSEPHAT HASSUNGA KUHUSU UZINDUZI WA MKAKATI WA KUENDELEZA ZAO MPUNGA
HOTUBA YA MGENI RASMI WAZIRI WA KILIMO MH. JOSEPHAT HASSUNGA KUHUSU UZINDUZI WA MKAKATI WA KUENDELEZA ZAO LA MPUNGA AWAMU YA PILI NCHINI, TAREHE 16 DESEMBA, 2019 - KATIKA UKUMBI WA ST. GASPAR ULIOPO JIJINI DODOMA.
Napenda kuwashukuru waandaaji wa tukio hili hususan Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) ambao wamekuwa nguzo kubwa kwetu katika kufanikisha shughuli mbalimbali za maendeleo hapa nchini ikiwemo maandalizi ya Mkakati huu nitakaouzindua rasmi leo.
Aidha, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kabisa kwa wenzetu wa HELVETAS, IRRI, BRiTEN RIKOLTO na AGRICOM ambao wamechangia kwa kiasi kikubwa kuweza kufanikisha uandaaji wa Mkakati huu na kufanikisha shughuli ya leo. Niwaombe muendelee kudumisha ushirikiano uliopo kati yenu na Wizara ya Kilimo katika kufanikisha maendeleo ya kilimo nchini na kuinua uchumi wa wananchi na Taifa kwa ujumla, hususan katika wakati huu tunapojizatiti kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025.