MWELEKEO WA MSIMU WA MVUA
Katika taarifa hiyo; TMA ilieleza kuwa katika kipindi cha Novemba, 2020 hadi Aprili, 2021 mvua za wastani hadi juu ya wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi yanayopata mvua za msimu mmoja kwa mwaka isipokuwa maeneo ya mkoa wa Kigoma, Katavi na magharibi mwa mkoa wa Tabora yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani kama zilivyo ainishwa kwenye Kielelezo Na.1.
Mvua hizo zinatarajiwa kuanza mapema kati ya wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Novemba, 2020 katika maeneo mengi isipokuwa maeneo machache ya mkoa wa Kigoma na Rukwa zinakotarajiwa kuanza wiki ya tatu ya mwezi Novemba, 2020. Aidha, mvua hizo zinatarajiwa kuisha kwa wakati katika wiki ya nne ya mwezi Aprili, 2021 katika maeneo mengi isipokuwa maeneo machache ya Mkoa wa Ruvuma yanayotarajiwa kuisha mapema kati ya wiki ya pili na ya tatu ya mwezi aprili, 2021.