Serikali ya Tanzania na Misri zinatarajia kusainiana mkataba wa makubaliano wa kuanzisha mashamba ma

Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga akiwa sambamba na Waziri wa Kilimo na Ardhi wa Misri Mhe. Dkt. Ezzidine Abu Stiet wakati wa majadiliano na Wataalam kutoka Wizara ya Kilimo Tanzania na Wataalam wa Wizara ya Kilimo ya Misri katika Ukumbi wa Wizara (Kilimo IV) Jijini Dodoma


 

Serikali ya Tanzania na Misri zinatarajia kusainiana mkataba wa makubaliano wa kuanzisha mashamba makubwa ya pamoja kwa lengo la kuinua kilimo cha ngano, mpunga na pamba


 

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga mara baada ya kufanya mazungumzo na timu ya Wataalamu wa kilimo kutoka Misri wakiongozwa na Waziri wa Kilimo na Ardhi wan chi hiyo, Dk Ezzidine Abu Stiet.


 

Mhe. Hasunga amesema katika mazungumzo hayo wamekubaliana kushirikiana katia Sekta ya Kilimo husan katika mazao ya mpunga, ngano na pamba ambapo tande zote mbili zitakuwa na mashamba ya pamoja.

 

“Kama mnavyojua Misri wamepiga hatua katika kilimo hususani kilimo cha umwagiliaji na tekinolojia hivyo tumekubaliana mafaniko hayo yahamie hapa nchini.”

 

Waziri Hasunga aliongeza: “Baada ya mazungumzo ya kina na makubaliano katika maeneo ya ushirikiano, tumepeana miezi miwili ili ifikapo mwezi Mei mwaka huu, tutasaini mkataba wa makubaliano na kuanza utekelezaji.

 

Amesema eneo lingine ambapo wamekubaliana ni kuimarisha Vituo vya Utafiti wa mazao ili kupata mbegu bora na namna bora ya kuzitumia mbegu hizo na pia kuhamisha ujuzi na zana kutoka Misri ambao utasidia kuinua kilimo hapa nchini.

 

Waziri Hasunga alisema kwa sasa Wataalam wa kilimo wa nchi hizo mbili watatumia muda huu wa miez miwili kutembelea maeneo mbalimbali ili kubainisha maeneo ambayo yanafaa kwa kilimo.

 

“Mfano tuliwaza kupeleka kilimo cha ngano wilayani Misenyi mkoani Kagera lakini wamesema eneo hilo ni dogo, hivyo wataalamu wa Misri na wale wa Tanzania watapita maeneo mbalimbali kuangalia maeneo yanayofaa na baadaye tusainiane mkataba wa makubaliano,” alisema.

 

Naye Waziri wa Kilimo na Ardhi wa Misri, Stiet alisema wamekuwa na mazungumzo mazuri na yenye mafanikio na kukubalianakushirikiana katika mafunzo, utafiti na tekinolojia katika sekta ya kilimo ili kuboresha mazao ya kimkakati ya pamba, mbunga na ngano..

 

“Makubaliano hayo yanaongeza wigo wa ushirikiano kati ya nchi hizi mbili ambayo ni ya muda mrefu, tumekubaliana kuinua kilimo katika mazao matatu kwa manufaa ya wananchi wa Tanzania. Baada ya kusainiana mkataba tunategemea utekelezaji wa haraka,” alimalizia.