CHONGOLO:: UBORA WA KAHAWA, NGUZO YA USHINDANI KATIKA MASOKO
Wadau wa tasnia ya Kahawa nchini wamehimizwa kuhakikisha wanazalisha Kahawa yenye ubora ili kuongeza upatikanaji endelevu wa masoko katika tasnia hiyo.
Wito huo umetolewa na Mhe. Daniel Chongolo (Mb), Waziri wa Kilimo tarehe 5 Juni 2026, wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 16 wa Wadau wa Kahawa uliofanyika tarehe 4-5 Juni, 2026 katika Ukumbi wa Hoteli ya St. Gasper, jijini Dodoma.
Waziri Chongolo amesema tasnia ya kahawa ina mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa Taifa kupitia mapato ya fedha za kigeni na kuboresha maisha ya wananchi wanaojihusisha na uzalishaji wa zao hilo. Amesema katika msimu uliopita, zao la Kahawa liliingizia Tanzania Dola za Marekani milioni 400.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Kahawa Tanzania, Prof. Aurelia Kamuzora amesema Tasnia ya Kahawa imeendelea kuwa kivutio kikubwa kwa kuwa mifumo ya mauzo ya Kahawa imeendelea kusambazwa katika mikoa mbalimbali nchini, hatua inayochangia kuongeza uwazi, ushindani na upatikanaji wa masoko kwa wakulima.
Naye Mbunge wa Jimbo la Kyerwa, Mhe. Khalid Mussa Nsekela, akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, amesema ongezeko la uzalishaji wa Kahawa barani Afrika linahitaji wakulima kupewa elimu na mbinu bora za uzalishaji ili kuongeza tija na kukidhi mahitaji ya soko la Dunia.
Aidha, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Kahawa Tanzania, Bw. Primus Kimaryo amebainisha kuwa uzalishaji wa zao hilo nchini umeongezeka kutoka tani 55,000 hadi tani 86,000 katika msimu uliopita, huku lengo likiwa ni kufikia tani 300,000 ifikapo mwaka 2030.
Mkutano Mkuu wa 16 wa Wadau wa Kahawa umewakutanisha wadau zaidi ya 400 kutoka mikoa takribani 17 nchini, wakiwemo Wakuu wa Mikoa inayozalisha Kahawa nchini ikiwemo Arusha, Ruvuma, Songwe, Njombe, Kigoma, Kagera; Waheshimiwa Wabunge, Wakulima, Vyama vya Ushirika, n.k. Kauli mbiu ya Mkutano ni “Uimarishaji wa Mfumo wa Ufuatiliaji kwa Upatikanaji wa Masoko na Ukuaji Endelevu.”