Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

CHONGOLO: WAKULIMA ONDOENI WASIWASI MBOLEA IPO

Imewekwa: 05 Jun, 2026
CHONGOLO: WAKULIMA ONDOENI WASIWASI MBOLEA IPO

Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo (Mb), amewahakikishia wakulima nchini kuwa mbolea ipo ya kutosha na inapatikana kukidhi mahitaji ya msimu wa kilimo unaoendelea na msimu ujao.

Akizungumza wakati wa ziara yake ya kukagua maghala ya waagizaji wa mbolea jijini Dar es Salaam tarehe 3 Juni 2026, Mhe. Chongolo ameeleza kuwa ametaka kujiridhisha kuhusu hali ya upatikanaji wa mbolea nchini na kuwathibitishia wananchi kuwa maandalizi ya pembejeo kwa ajili ya uzalishaji yanaendelea vizuri hivyo wasiwe na hofu. 

Ametolea mfano wa kampuni ya ETG ambayo pekee ina zaidi ya tani 47,000 za mbolea ambazo tayari zimesambazwa katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo mikoa ya Mbeya, Iringa na Kilimanjaro, huku shehena za mbolea zikiendelea kupakiwa na kusambazwa katika maeneo mengine nchini.

“Tumekuja kutembelea waagizaji wa mbolea ili kujiridhisha kuhusu uwepo wa mbolea. Hata katika kipindi hiki ambacho shughuli za  kilimo zimepungua kwa maeneo mengi, tumebaini kuwa mbolea ipo ya kutosha na itaendelea kupatikana kwa msimu huu na msimu ujao wa kilimo,” amesema Mhe. Chongolo.

Waziri Chongolo amesema kuwa Serikali inaendelea kutekeleza Mpango wa Ruzuku ya Mbolea unaolenga kuhakikisha mkulima hapungukiwi pembejeo muhimu, huku timu maalum zikiendelea kufanya ufuatiliaji nchi nzima kujiridhisha kuwa mbolea inapatikana na kuwafikia wakulima kwa wakati.

Katika hatua nyingine, Mhe. Chongolo alitoa onyo kwa watu wanaojihusisha na udanganyifu au uchakachuaji wa pembejeo za kilimo, akisisitiza kuwa Serikali ipo macho na haitasita kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya yeyote atakayebainika kuhujumu Sekta ya Kilimo kwa kuuza pembejeo zisizokidhi viwango.