Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

KATIBU MKUU MWELI AALIKA KAMPUNI ZA BELARUS KUWEKEZA TANZANIA

Imewekwa: 03 Jun, 2026
KATIBU MKUU MWELI AALIKA KAMPUNI ZA BELARUS KUWEKEZA TANZANIA

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli ametembelea Viwanja vya Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo ya Jamhuri ya Belarus (BELAGRO - 2026) tarehe 3 Juni 2026 nchini humo, na kufanya mazungumzo na Bw. Valery Ivankovich, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Minsk Automobile Plant (MAZ OJSC) inayohusika na utengenezaji wa magari ya kusafirisha nafaka na mazao ya bustani ambayo yana miundombinu ya uhifadhi wa chakula.

Wakati akitembelea na kujionea magari ya Kampuni hiyo, Katibu Mkuu Mweli alikaribisha Kampuni hiyo kuja kuwekeza nchini kwa kufanya majaribio ya teknolojia inazozalisha kutokana na uhitaji wa magari ya aina hiyo.  Amewaeleza pia kuhusu ongezeko la uzalishaji wa mazao ya mbogamboga na matunda (horticulture) hususan zao la parachichi ambapo kumekuwa na changamoto ya usafirishaji wake hadi kufikia bandarini. 

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu Mweli amefanya mazungumzo na Bw. Aleksandr Efimov, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya AMKODOR OJSC inayotengeneza mashine za kilimo, zikiwemo za maandalizi ya shamba na uhifadhi wa mazao baada ya kuvunwa.

Kufuatia kuvutiwa na ubora wa mashine za kampuni hiyo, Katibu Mkuu Mweli ameikaribisha Kampuni hiyo kuja nchini kuwekeza kwa kuanza na majadiliano ili wadau wapate elimu zaidi ya mashine zao kabla ya kuziingiza sokoni.