SILINDE AZITAKA COPRA NA TMX KUSIMAMIA UUZAJI WA MAZAO YA KIMKAKATI KUPITIA USHIRIKA
Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) na Soko la Bidhaa Tanzania (TMX) zimetakiwa kuhakikisha mazao ya kimkakati yanayozalishwa na Wanaushirika yanakusanywa na kuuzwa kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani kwa Vyama vya Ushirika pekee, badala ya wanunuzi binafsi.
Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde (Mb), amesema hayo wakati akifunga Jukwaa la Tano la Maendeleo ya Ushirika Mkoa wa Dodoma tarehe 6 Juni 2026, jijini Dodoma alimwakilisha Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo (Mb).
Mhe. Silinde amesema mfumo wa ushirika umeendelea kuthibitika kuwanufaisha zaidi wakulima, hivyo ni muhimu kuhakikisha mazao ya kimkakati yanauzwa kupitia vyama vya ushirika ili kuongeza tija na manufaa kwa wazalishaji.
Aidha, amezitaka COPRA na TMX kutafuta njia mbadala za kuboresha bei za mazao kufuatia malalamiko ya wakulima kuhusu bei za kuanzia kwenye minada kuwa ndogo na kutokidhi matarajio yao, amesema taasisi hizo zinapaswa kuhakikisha wakulima wanapata bei nzuri na zenye kuridhisha ili kunufaika ipasavyo na uzalishaji wao.
Naibu Waziri huyo amesema Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kisera na kisheria kwa lengo la kuimarisha Ushirika nchini, huku ikihakikisha wakulima wanazalisha mazao yenye ubora wa ushindani katika soko la ndani na la nje.
Vile vile, ameitaka Benki ya Ushirika kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa Vyama vya Ushirika na Wanaushirika binafsi ili kuongeza uzalishaji na tija katika Sekta ya Kilimo.