Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

TANZANIA YAFUNGUA FURSA ZA UWEKEZAJI KWA BELARUS

Imewekwa: 04 Jun, 2026
TANZANIA YAFUNGUA FURSA ZA UWEKEZAJI KWA BELARUS

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Mweli amefanya mazungumzo na Waziri wa Viwanda wa Jamhuri ya Belarus, Mhe. Andrew Kuznetsov, tarehe 4 Juni 2026 nchini humo. 

Viongozi hao wamejadili kuimarisha ushirikiano katika Sekta ya Kilimo hususan kubadilishana ujuzi na uzoefu katika maeneo ya teknolojia za matrekta, mashine za kuchakata mazao ya kilimo; ikiwa ni pamoja na kujengeana uwezo kwenye maeneo ya ubunifu wa teknolojia mbalimbali za mashine za kilimo kwenye mnyororo wa uzalishaji mazao.

Sambamba na hayo, pia wamejadiliana kuanzisha programu za kubadilishana wataalam kwa nchi hizo mbili, hatua itakayozalisha na kuongeza wataalam, pamoja na kuwezesha vijana wa Kitanzania kupata ujuzi na maarifa katika kubuni na kutengeneza mashine za kilimo kwa kutumia teknolojia rahisi na za kisasa zitakazozalisha ajira kwa vijana.

Katika mwendelezo wa mazungumzo yao, Katibu Mkuu Mweli amemuomba Waziri wa Viwanda wa Belarus kuhamasisha kampuni za nchi hiyo kuja kuwekeza nchini ili zinufaike na fursa ya unafuu wa kodi kwa wawekezaji wa nje na kwa kuwa Tanzania ni mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Mkataba wa Uanzishwaji wa Eneo Huru la Biashara Africa (AfCFTA) ambapo kutawapa fursa kubwa ya kufanya biashara na zaidi ya nchi 25 zilizowanachama wa EAC na SADC.