Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

WAKULIMA NA WAFANYABIASHARA KUTOKA BELARUS WAKARIBISHWA KUSHIRIKI MAONESHO YA NANE NANE 2026

Imewekwa: 08 Jun, 2026
WAKULIMA NA WAFANYABIASHARA KUTOKA BELARUS WAKARIBISHWA KUSHIRIKI MAONESHO YA NANE NANE 2026

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli amefanya mazungumzo na Waziri wa Kilimo wa Jamhuri ya Belarus, Mhe. Yury Gorlov, tarehe 6 Juni 2026 kwa lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya Wizara hizo kufuatia Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) iliyosainiwa Julai 2025. 

Viongozi hao pia wamejadili ushirikiano wa kufanya biashara ya mazao ya kilimo ambapo Katibu Mkuu Mweli ameeleza kuwa Tanzania iko tayari kufanya biashara ya mazao ya Kahawa, Korosho, Chai, Parachichi na mazao ya viungo.

Pia, Katibu Mkuu Mweli ameeleza kuhusu fursa iliyopo katika uwekezaji wa viwanda vya mbolea Tanzania kwa kubainisha mahitaji ya mbolea ya nchini pamoja na nchi zinazoizunguka Tanzania katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Waziri wa Kilimo wa Jamhuri ya Belarus amealikwa na wafanyabiashara wa bidhaa za kilimo kutembelea Tanzania ili kushiriki katika Maonesho ya Kimataifa ya Nane Nane 2026 kwa kuleta na kuonesha bidhaa na teknolojia za kilimo za nchi hiyo yakiwemo  matrekta na zana zake, mashine za uongezaji thamani na uhifadhi wa mazao. 

Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo wa Jamhuri ya Belarus alitoa mwaliko mwa Katibu Mkuu Mweli kuleta wataalam wa kilimo nchini Belarus ili wakajifunze na kujengewa uwezo wa uendeshaji na usimamizi wa teknolojia mbailmbali za kilimo katika mnyororo wa uzalishaji mazao ya kilimo.