ZAIDI YA MIKOA 6 YAFIKIWA UPIMAJI WA AFYA YA UDONGO
Zaidi ya Mikoa sita imefikiwa katika zoezi la upimaji wa afya ya udongo kitaifa ambayo ni pamoja na Mikoa ya Rukwa, Katavi, Songwe, Mbeya,Iringa na Njombe.
Zoezi hilo limeanza tarehe 3 Juni 2026 ambapo wataalam wanakusanya na kuchambua sampuli za udongo ili kuwezesha uandaaji wa ramani za kidijitali zitakazobainisha hali ya udongo na mazao yanayofaa kulimwa katika maeneo mbalimbali.
Zoezi hili linahusisha wataalamu kutoka Wizara ya Kilimo; Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI); Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB); Bodi ya Mkonge Tanzania; Chuo cha Sukari cha Taifa; Vyuo vya Mafunzo ya Kilimo (MATI); Maafisa Kilimo wa Serikali za Mitaa; wataalamu pamoja na wahitimu kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA); Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA).
Akizungumza wakati wa utekelezaji wa zoezi hilo, Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Usimamizi wa Matumizi ya Ardhi ya Kilimo kutoka Wizara ya Kilimo, Mha. Florian Kalemela, amesema kuwa upimaji wa afya ya udongo ni sehemu ya utekelezaji wa kiashiria na. 7, kinacholenga kuhakikisha taarifa sahihi za kisayansi zinapatikana ili kusaidia maendeleo ya Sekta ya Kilimo nchini.
Amesema sehemu ya kwanza ya utekelezaji wa kiashiria hicho ni kufanya tathmini ya afya ya udongo na kuandaa mipango ya matumizi sahihi ya mbolea kulingana na mahitaji halisi ya maeneo husika. Mha. Florian ameeleza zaidi kuwa sampuli za udongo hupelekwa maabara kwa ajili ya uchambuzi. Baada ya matokeo kutoka, huwekwa katika ramani za kidijitali ambazo zitawezesha kuonesha hali ya afya ya udongo katika maeneo husika, pamoja na kubainisha ni mazao gani yanafaa kulimwa katika maeneo mbalimbali.
“Katika Mkoa wa Rukwa kuna jumla ya maeneo ya uchunguzi (observation points) 1963, ambapo kuna mashimo ya uchunguzi wa udongo 205 yanayochimbwa kwa ajili ya kufanya tathmini ya kina ya tabaka mbalimbali za udongo. Wastani kila shimo huwa na tabaka kati ya tatu na nne. kwa ajili ya uchambuzi wa maabara,” amesema Mha. Kalemela.
Wizara ya Kilimo tayari imeshapima afya ya udongo katika mikoa 19 nchini.