Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

JOPO LA WAWEKEZAJI WA UJERUMANI KUSHIRIKI MAONESHO YA NANE NANE 2026

Imewekwa: 18 Jan, 2026
JOPO LA WAWEKEZAJI WA UJERUMANI KUSHIRIKI MAONESHO YA NANE NANE 2026

Jopo la Wafanyabiashara na Wawekezaji kutoka nchini Ujerumani (German Agribusiness Alliance) laahidi kushiriki katika Maonesho ya Kitaifa na Kimataifa ya Wakulima ya Nane Nane nchini Tanzania mwezi Agosti 2026. 

Jopo hilo limetoa ahadi hiyo tarehe 16 Januari 2026 wakati wa Mkutano kati ya Tanzania na Wafanyabiashara / Wawekezaji (Tanzania Business/Investment Roundtable Meeting) ulioongozwa na Mhe. Daniel Chongolo (Mb), Waziri wa Kilimo pembezoni mwa ushiriki wa Tanzania katika Jukwaa la Kimataifa la Chakula na Kilimo (GFFA) linalofanyika nchini Ujerumani. 

Wakati wa mkutano huo, Tanzania iliwasilisha mada za kuvutia uwekezaji katika maeneo makuu matatu ambayo ni uwekezaji kwenye kukuza uzalishaji na uchakataji katika mazao ya mbegu za mafuta (Alizeti na Chikichi), Ngano, na Soya; kupanua biashara ya mazao ya Kokoa, Kahawa na Korosho; uwekezaji kwenye miundombinu ya uhifadhi na usafirishaji mazao ya horticulture na zana za kilimo likihusisha pamoja na umwagiliaji.  

Aidha, Mhe. Waziri Chongolo alitoa mwaliko kwa jopo hilo kushiriki katika Maonesho ya Nane Nane yanayotarajiwa kuanza tarehe 01 hadi 08 Agosti 2026 ili kutumia fursa hiyo kujifunza zaidi jinsi Tanzania inavyokutanisha Wakulima, Wafugaji na Wadau mbalimbali katika mnyororo wa thamani wa Sekta hizo ili kufanya biashara, uwekezaji, kubadilishana uzoefu katika matumizi ya teknolojia za zana za kilimo na maeneo mengine.  

Kwa upande wake, Bw.  Frank Karl Nordmann, Mwenyekiti wa German Agribusiness Alliance ametoa shukran kwa mwaliko huo na kuahidi jopo hilo kushiriki katika Maonesho ya Nane Nane 2026 na kutumia fursa hiyo kwa ajili ya hatua za kuanza uwekezaji na biashara nchini Tanzania katika mazao ya Viazi, Kokoa, mashine na zana za kilimo.  

Katika hatua nyingine, Bw. Gerald Mweli, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo ameshiriki katika Hafla ya Jioni ya German AgriBusiness Alliance ambapo amechangia hatua mbalimbali za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuongeza tija na uzalishaji wa mazao kwa wakulima.  “Dhamira ya Tanzania ni kukuza wigo katika uwekezaji, na tuna fursa za uchakataji, zana za kısasa za kilimo (mechanization), na mifumo ya kidigitali katika kilimo ambapo amekaribisha wawekezaji kuchangamkia  katika Sekta ya Kilimo hususan maeneo ya kimkakati.  Karibuni sana Tanzania,” ameongeza Katibu Mkuu Mweli.