Wataalamu wanaohusika na zoezi la ukusanyaji wa sampuli za udongo kwa ajili ya upimaji wa afya ya udongo nchini, wamefanya kikao kazi kinacholenga kujadili na kutoa elimu ya namna bora ya ukusanyaji wa sampuli za udongo, kwa ajili ya upatikanaji wa ramani ya afya ya udongo kidigitali pamoja na usimamizi sahihi wa ardhi ya kilimo.
Kikao kazi hicho kimefanyika tarehe 6 Januari 2026 mkoani Morogoro na kuhusisha wataalamu kutoka Wizara ya Kilimo; Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI); Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB); Bodi ya Mkonge Tanzania; Chuo cha Sukari cha Taifa; Vyuo vya Kilimo ( MATI); maafisa kilimo; wataalamu kutoka Chuo cha Kilimo cha Sokoine ( SUA); Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA); pamoja na wahitimu kutoka katika vyuo mbalimbali nchini.
Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo (Mb), amekutana na wawekezaji kutoka Kampuni ya Shandong Wanda Xing Automobile ya nchini China kujadili uwekezaji katika Sekta ya Kilimo hususan kuongeza uzalishaji wa mazao, thamani na kuleta teknolojia za kisasa zitakazoleta tija kwa wakulima.
Mkutano huo umefanyika tarehe 05 Januari 2026, jijini Dar es Salaam ambapo wawekezaji hao wameonesha nia ya kuwekeza katika mazao ya kimkakati, likiwemo zao la Korosho, kuanzia uzalishaji hadi uongezaji wa thamani wa zao hilo.