MAWAZIRI WA KILIMO DUNIANI WASHUHUDIA UFUNGUZI WA WIKI YA KIJANI NCHINI UJERUMANI
Rais wa Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani, Mhe. Frank-Walter Steinmeier amefungua rasmi Maonesho ya Kimataifa ya Wiki ya Kijani (Green Week) ambayo kwa mwaka huu yametimiza miaka 100 tangu kuanzishwa kwake katika mji wa Berlin mwaka 1926 nchini Ujerumani.
Maonesho hayo yana kauli mbiu ya “Water. Harvests. Our Future” yanashabihiana na Maonesho ya Wakulima ya Kitaifa na Kimataifa ya Nane Nane yanayofanyika chini Tanzania kila mwaka katika wiki ya kwanza ya mwezi Agosti.
Akihutubia ufunguzi huo mjini Berlin, Mhe. Rais Frank-Walter Steinmeier ameeleza kuvutiwa sana na mabadiliko ya kiteknolojia katika Sekta ya Kilimo na ana matumaini kuwa Sekta hiyo itazidi kuleta mageuzi yenye mchango mkubwa katika kukabiliana na mahitaji ya chakula Duniani katika miaka ya mbele.
Kuhusu siasa za kilimo na usalama wa chakula kwa kuzingatia umuhimu wa maji katika kilimo, Mhe. Rais Frank-Walter Steinmeier amesema ni muhimu Mataifa ya Ulaya na Wadau muhimu katika mnyororo wa thamani wa kilimo kushirikiana katika kukuza Sekta ya Kilimo hususan katika kusaidia Wakulima wadogo. Amesisitiza kuwa pia ni muhimu kutafuta Wadau wapya katika kushirikiana na kukuza Sekta hiyo kwa kuwa inakuwa kwa kasi.
“Sekta ya Kilimo ni muhimu sana katika siasa za Dunia. Kila bidhaa inayoonekana katika maduka, inaanzia kutoka shambani na kufuatia na mnyororo mzima wa uzalishaji. Hivyo, ni muhimu kusaidia Wakulima na kuhakikisha wanapata unafuu katika uzalishaji na kujijengea uhimilivu wa mabadiliko ya tabianchi kupitia teknolojia bunifu na upatikanaji wa masoko,” ameongeza Mhe. Frank-Walter Steinmeier.
Ufunguzi huo umehudhuriwa na Washiriki zaidi ya 500 kutoka Mataifa mbalimbali Duniani, akiwemo Mhe. Alois Rainer, Waziri wa Kilimo, Chakula na Utambulisho wa Kikanda (Minister for Agriculture, Food and Regional Identity), ukiwemo ujumbe wa Sekta ya Kilimo kutoka Tanzania ulioongozwa na Mhe. Daniel Chongolo (Mb), Waziri wa Kilimo.