Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

MIRADI YA UMWAGILIAJI KUNUFAIKA NA VITENDEA KAZI VYA SHILINGI BILIONI 23.4

Imewekwa: 29 Jan, 2026
MIRADI YA UMWAGILIAJI KUNUFAIKA NA VITENDEA KAZI VYA SHILINGI BILIONI 23.4

Serikali imekabidhi vitendea kazi vyenye thamani ya shilingi bilioni 23.4 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya Umwagiliaji , huku Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) ikipongezwa kwa kuwa nguzo ya uchumi wa Taifa. 

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo (Mb) amesema “Serikali iliongeza bajeti ya maendeleo kutoka shilingi bilioni 46.5 mwaka 2021/22 hadi shilingi bilioni 308.7 mwaka 2025/26. Wizara itaendelea kusimamia na kufuatilia upatikanaji wa fedha ili ikamilike kwa wakati,” huku akiielekeza Bodi ya Uongozi ya NIRC na watumishi wa NIRC kusimamia vizuri rasilimali hizo.

Vitendea kazi hivyo ni pamoja na mitambo mikubwa 19 ya kuchimba visima vyenye uwezo wa kufikia urefu wa mita 300 hadi 1800, magari 17 ya kubeba vifaa na malighafi, trela 2 na pikipiki 23.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NIRC, Bw. Raymond Mndolwa amesema kuwa vifaa hivyo niutekelezaji wa agizo la Mhe. Rais Dkt. Samia alilolitoa Agosti 8, 2022 la kutaka mitambo mikubwa ya visima 19, magari 16, trela 2 na pikipiki 23 kusaidia shughuli za kilimo.  

“Tume imepanga kuchimba visima 67,000 ndani ya miaka 5, vitakavyohudumia hekta 16,000. Katika mwaka huu wa fedha pekee, visima 1,027 vimepangwa kuchimbwa na tayari visima 260 vimeshachimbwa kwa majaribio katika mikoa 12,” ameeleza Bw. Mndolwa. 

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, amesema kuwa asilimia 72 ya wananchi wa mkoa huo wanategemea kilimo, hivyo ujio wa vifaa hivyo ni mapinduzi makubwa ya kiuchumi.

Aidha, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, Mhe. Mariam Ditopile (Mb), pamoja na Katibu wa CCM Mkoa wa Dodoma, Mhe. Pili Mbaga wametoa pongezi kwa Serikali na Mhe. Rais Dkt. Samia kwa kuwekeza katika kilimo cha umwagiliaji kwa vitendo.