Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

NAIBU WAZIRI SILINDE ARIDHISHWA NA MIRADI YA UMWAGILIAJI TABORA NA SINGIDA

Imewekwa: 13 Jan, 2026
NAIBU WAZIRI SILINDE ARIDHISHWA NA MIRADI YA UMWAGILIAJI TABORA NA SINGIDA

Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde (Mb) ameridhishwa na miradi ya ujenzi na upanuzi wa miundombinu ya umwagiliaji inayoendelea mikoa ya Tabora na Singida kufuatia ziara yake ya ukaguzi tarehe 11 Januari 2026.

Akiwa mkoani Tabora katika Skimu ya Umwagiliaji ya Mwamapuli, Naibu Waziri Mhe. Silinde alishuhudia mafanikio makubwa yaliyopatikana kwa wakulima wa mpunga kupitia Chama cha Ushirika cha Umwagiliaji Maji Mwamapuli (AMCOS). Chama hicho kina wanachama 970, wakiwemo wanawake 270 na wanaume 700.

Mwenyekiti wa Chama hicho, Bw. Ramadhani Muna Ngella, amesema kuwa wakulima wamefanikiwa kuongeza uzalishaji wao kutoka tani 2.5 hadi tani 7.5 kwa hektari moja. Mafanikio hayo yametokana na upatikanaji wa maji ya uhakika, matumizi sahihi ya mbolea na ufuataji wa kanuni bora za kilimo.

Chama hicho kimefanikiwa kumiliki zana mbalimbali za kisasa za kilimo ikiwemo trekta moja, rotaveta moja, mashine tatu za kuvunia mpunga pamoja na mashine ya kukoboa mpunga, hatua iliyopunguza gharama za uzalishaji na kuongeza ufanisi kwa wakulima.

Nao Wakulima wa Mwamapuli wameipongeza Serikali ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwaunga mkono kupitia ruzuku ya mbolea na upanuzi wa skimu ya umwagiliaji uliowanufaisha pia vikundi vya Mahambasi A, Mahambasi B, Makomero A na Makomero B kwa kujengewa mitaro na barabara za mashambani.

Aidha, Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ilieleza kuwa mradi wa upanuzi wa Skimu ya Mwamapuli unaongeza eneo la umwagiliaji kutoka hekta 630 hadi hekta 2,565, na unatarajiwa kuwanufaisha wakulima wapatao 5,000, hatua itakayoongeza uzalishaji na kipato kwa wananchi wengi zaidi.

Katika mkoa wa Singida, Naibu Waziri wa Kilimo alitembelea mradi mkubwa wa umwagiliaji wa Msingi unaotekelezwa katika Kijiji cha Ishinsi, wilaya ya Mkalama. Mradi huo unaogharimu shilingi bilioni 34 unatarajiwa kumwagilia zaidi ya ekari 2,000 na kunufaisha wakulima 5,000 pamoja na wakazi zaidi ya 12,000 wa vijiji nane.

Wakulima wanatarajiwa kuongeza uzalishaji wa mazao mbalimbali ikiwemo mpunga, mahindi, alizeti na vitunguu, huku uzalishaji wa mpunga ukitarajiwa kufikia gunia 45 hadi 50 kwa ekari moja.